Friday, 8 June 2018

WANAWAKE 363 KIJIJINI MLANDA WAPATA HATI MILIKI ZA ARDHI
WANAWAKE 363 sawa na asilimia 48 ya wananchi 772 waliopata hati miliki za kimila 1,777 katika kijiji cha Mlanda wilayani Iringa wamesema, hatua hiyo italinda umiliki wa ardhi waliyopata ambayo awali usimamizi na manufaa yake yaliwalenga zaidi wanaume katika familia zao.

Hati hizo zimetolewa kupitia Mradi wa Urasimishaji Ardhi (LTA) unaotekelezwa katika vijiji 36 vya wilaya hiyo chini ya Mpango wa Kupunguza Njaa na Utapiamlo (Feed the Future) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).

Akiwakabidhi hati hizo kijijini hapo hivikaribuni, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya aliupongeza mradi huo akisema umejenga uelewa wa haki za wanawake na jamii katika kumiliki ardhi na umesaidia kuwahamasisha kutumia nafasi waliyopewa kuomba ardhi ambayo ni rasilimali muhimu katika kukuza kipato chao.

Mmoja wa wanawake walionufaika na mpango huo, Zilpa Mgata alisema wanafurahi kuona mila na desturi zilizokuwa zikiwanyima haki ya kumiliki ardhi katika jamii zao zinapoteza nguvu zake mbele ya sheria mbalimbali za ardhi. 

“Tumeelimishwa jinsi sheria hizo zinavyoondoa tofauti za umiliki wa ardhi baina ya mwanamke na mwanaume, jamii inajua na imeanza kuuona umuhimu wa mwanamke kutobaguliwa katika umiliki wa ardhi,” Mgata alisema na kueleza jinsia atakavyokitumia ardhi aliyomilikishwa yenye ukubwa wa heka tatu kutafuta mikopo na kuwekeza katika shughuli za kilimo na ufugaji.

Awali Naibu Mkurugenzi wa LTA, Malaki Msigwa alikipongeza kitengo chao cha uelimishaji akisema kimewazindua wanawake wengi kuelewa haki yao ya kumiliki ardhi na kutumia sheria hizo kupata haki hiyo.

“Hili ni jambo la kujipongeza sana ni jambo linaloonesha mafanikio makubwa katika jamii zetu. Sio suala la mchezo leo hii kushuhudia asilimia 48 ya wananchi waliopata hati hizi zinazowapa haki ya kumiliki ardhi ni wanawake,” alisema.

Mbali na wanawake hao, Msigwa alisema wanaume 409 sawa na asilimia 52 ya wananchi hao nao wamenufaika na mpango huo unaothibitisha umiliki na utumiaji wa ardhi kwa mmiliki, unaopunguza migogogo, unaomlinda mmiliki kulipwa fidia na unaomuwezesha kuitumia kama dhamana mahakamani au katika taasisi za fedha kuomba mikopo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Vitalis Samila alisema kijiji cha Mlanda kipo katika kata ya Magulilwa, tarafa ya Mlolo, umbali wa Kilometa 25 kutoka mjini Iringa.

Akizungumzia utekelezaji wa mpango huo kwa ngazi ya wilaya alisema, mradi huo utakaotekelezwa hadi Novemba 2019, umekamilisha matumizi bora ya ardhi katika vijiji 28 tangu utekelezaji wake uanze Januari 2016, umepima vipande vya ardhi 40,000 na umeshatayarisha hati 37,000.

Msigwa alisema mradi umepokea ombi la halmashauri hiyo la kutekeleza mpango huo katika vijiji 97 vilivyobaki na unaendelea kulifanyia kazi.

Ombi hilo lilitolewa na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo aliyetaka halmashauri yake iwe ya kwanza na ya mfano nchini kwa kuwa na vijiji vyote vyenye mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment