Monday, 4 June 2018

DAKTARI AFAFANUA KILICHOKATISHA UHAI WA MAPACHA WALIOUNGANA

Image result for MAPACHA WALIOUNGANADAKTARI bingwa wa magonjwa ya ndani wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa, Dk Faith Kundi amezungumzia sababu zilizosababisha mapacha maarufu walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti kupoteza maisha kabla ya kufikia ndoto zao.

Moja ya ndoto waliyokuwa nayo mapacha hao ni kumaliza elimu yao ya chuo kikuu, na kutumia maarifa ambayo wangepata kusaidia jamii, wakiwemo watu wenye ulemavu.

Akizungumza na wanahabari mapema leo, Dk Kundi alisema Maria alikuwa na tatizo zaidi la kiafya ikilinganishwa na Consolota.

“Maria alikuwa na tatizo kubwa kwenye mapafu, mapafu yalikuwa yameharibika hali iliyomfanya asaidiwe na mashine ya Oksijeni kupumua,” alisema.

Alisema aliwapokea pacha hao Mei 17 majira ya saa 1.30 usiku wakitokea katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam walikokuwa wakitibiwa kwa zaidi ya miezi miwili.

“Wakati nikiwapokea, Maria alikuwa anatumia mashine ya Oksijeni lakini Consolata alikuwa anapumua kawaida na hali hiyo imeendelea hadi mauti yalipowakuta,” alisema.

Pamoja na tatizo la kupumua, Dk Kundi alisema Maria alikuwa na tatizo lingine wakati wa hedhi kwani ilikuwa inabaki ndani kwa ndani na haitoki kama inavyotoka kwa wanawake wengine.

“Pamoja na Maria kutumia Oksijeni muda wote, kwa pamoja walikuwa wanatumia dawa mbalimbali na walikuwa wakifanyiwa vipimo vingine mara kwa mara,” alisema.

Dk Kundi alisema hawezi kusema chochote kama kulikuwepo na uwezekano wa mapacha hao kutengenishwa wakati wa uhai wao na kunusuru maisha yao, kwani suala hilo linahitaji utafiti.

“Hata hivyo lazima nikiri kwamba Mungu amewapa nafasi ya pekee, wameishi miaka 21, sio jambo dogo kwa hali waliyokuwa nayo,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa taarifa waliyopewa toka Muhimbili, kwa hali iliyovyokuwa isingewezekana tena kwa Maria kupumua bila mashine ya Oksijeni kwa maisha yake yote yaliyobaki, na ndivyo ilivyokuwa hadi mauti ilipomfika na baadaye kumfika na pacha mwenzake. 

Mapacha hao walikufa Jumamosi iliyopita majira ya saa 2.30 na 3.00 usiku wakati wakiendelea na matibabu, Maria akitangulia na Consolatra akifuata ndani ya dakika 10 na 15 baadaye.

Mapacha hao wa kipekee walikuwa wameungana sehemu ya kiwiliwili, wakiwa na vichwa viwili, mioyo miwili na mikono minne.

Na walikuwa wanatumia viungo vingine kwa pamoja kama tumbo, ini, na sehemu ya uke na haja.

Pamoja na kwamba Maria anaelezwa kuwa na tatizo la kiafya tangu alipozaliwa  alikuwa na uwezo wa kula chakula zaidi ya mwenzake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela mapacha hao watazikwa Jumatano katika makaburi ya Shirika la Mtakatifu Maria Consolata, Tosamaganaga, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa.

Katika wosia wao walioutoa kwa Kiongozi Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Maria Consolata, Sista Jane Nugi wakati wakitibiwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, waliomba wazikwe katika makaburi ya masista wa shirika hilo katika kijiji cha Tosamaganga kutokana na mchango mkubwa walioutoa masista hao kwao.

Akizungumza na wanahabari jana Sista Jane alisema katika maisha yao yote watoto hao wamelelewa na kupewa huduma zingine muhimu kupitia shirika hilo.

“Watoto hao walikuwa sehemu ya familia ya masista na ndio maana walipewa majina ya ya shirika, Maria na Consolata. Kuondoka kwao kumeacha pengo kubwa sana kwa shirika hili na jamii inayowazunguka,” alisema.

Wakati huo huo baadhi ya ndugu wa mapacha hao ambao awali walidhaniwa kujificha kutokana na hali za mapacha hao wameanza kuwasili mjini Iringa kushiriki mazishi yao.

Pamoja na kaka yao mkubwa Davidi Mwakikuti wengine waliowasili ni mama yao mdogo Anna Mshumbushi, baba mkubwa, wajomba na dada yao Jackline Mwakikuti.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment