Friday, 8 June 2018

CHALAMILA AWAVAA WALIOANZA KAMPENI ZA UBUNGE, UDIWANI MUFINDI

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Albert Chalamila ametoa onyo kali kwa wana CCM walioanza kampeni za chini kuwania ubunge na udiwani katika majimbo matatu ya wilaya ya Mufindi akisema wanakwenda kinyume na kanuni za uongozi na maadili.

Majimbo hayo ni Mafinga Mji linaloongozwa na Mbunge Cosato Chumi, Mufindi Kaskazini Mahamudu Mgimwa na Mufindi Kusini Meldrad Kigolla.

Alitoa onyo hili jana, wakati akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya wilaya hiyo mjini Mafinga alipokuwa akielezea mwelekeo wake wa usimamizi wa shughuli za chama katika kipindi cha uongozi wake tangu ashike wadhifa huo mwishoni mwa mwaka jana.

Kwa kutumia macho yake na taarifa za vyombo vya chama na vya dola (Usalama wa Taifa) alisema ameanza kuwabaini baadhi ya wana CCM walioanza kujitengenezea mazingira kwa ajili ya kupata uteuzi katika uchaguzi mkuu ujao kinyume na kanuni hizo za chama.

Bila kuwataja majina, mwenyekiti huyo kijana aliwataka wana CCM hao kuanza kufuta ndoto hizo akisema chama kitatumia kanuni na katiba yake kuwaengua na ikiwezekana itawanyang’anya kadi mapema iwezekanavyo ili kuondoa mipasuko inayoweza kuwagharimu katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Katika mazingira ya kusikitisha alisema wana CCM wengine wanaoshiriki kuhatarisha amani ndani ya chama hicho ni wale waliopewa dhamana ya kuwa wajumbe wa vikao vikubwa vya chama na katika onyo lake kwao aliwatahadharisha dhidi ya hatua zinazoweza kuchukuliwa kwao.

“Waacheni wabunge na madiwani waliopo wafanye kazi, wamalize miaka yao mitano kwa uhuru. Mliwachagua wenyewe, wapeni nafasi na kama mnataka kuamua vinginevyo subirini hadi pazia la uchaguzi litakapofunguliwa lakini sio sasa,” alisema.

Katika mwelekeo wake mwingine, Chalamila alizungumzia visasi na mioyo ya kinyongo miongoni mwa wana CCM wakati na baada ya chaguzi za chama na jumuiya zake, na za serikali akisema; mambo hayo yamekuwa yakisabisha mpasuko wa muda mrefu ndani ya chama hivyo ni lazima yaachwe.

“Visasi na vinyongo vimevuka mipaka. Wapo pia wana CCM ambao kila kukicha kazi yao ni kuwazushia na kuwachafua wenzao kwamba ni wafuasi wa vyama vingine vya siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kwamba wana mienendo mibaya ndani ya chama mambo ambayo si ya kweli. Wana CCM tupendane na tutendeane mema,” alisema.

Aliwataka wenye taarifa za wanachama wenye mienendo mibaya na inayotishia uhai wa chama waziwasilishe kwa kuzingatia taratibu, kanuni na katiba ya chama ili ziweze kufanyiwa kazi.

Alitaja mwelekeo wake mwingine katika uongozi wake kuwa ni kuendesha chama kwa kuzingatia msingi wa siasa safi zisizo na majungu ili kulinda taswira ya mkoa wa Iringa ulioharibiwa na siasa za majungu huko nyuma.

Na katika kufikia lengo hilo, aliahidi pia kukutana na wabunge wote wa CCM wa mkoa wa Iringa ili wafahamu mwelekezo wake unaolenga kukifanya chama hicho kiwe cha wanachama wote.

“Huku nyuma kulikuwepo na baadhi ya wana CCM waliokuwa wakijinasibu kwamba wao ndio wenye chama na wana uwezo wa kuamua lolote bila maamuzi ya vikao vya chama. Kwa muda mrefu wana CCM hao walionekana watu wenye nguvu kuliko chama, nataka kuwaambia CCM ya sasa sio ya wakati ule, tunawasubiri wapiti kwenye reli, tuwashughulikie,” alisema.

Wakati huo huo Chalamila amewakumbusha wana CCM kujiandaa kwa uchaguzi wa mwakani wa Serikali za Mitaa akisema; “ni uchaguzi muhimu unaosaidia kutathimini utekelezaji wa Ilani ya chama kwa kuzingatia vipaumbele vyake na ndio unatoa dira ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2020.”

Baada ya kukutana na halmashauri kuu ya CCM ya wilaya ya Mufindi, Chalamila anatarajiwa pia kukutana na na wajumbe wa vikao hivyo wa wilaya ya Kilolo, Iringa Vijijini na Manispaa ya Iringa katika ziara yake anayofanya akiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Viti 15 Bara), Theresia Mtewele

Reactions:

0 comments:

Post a Comment