Sunday, 10 June 2018

CHALAMILA APIGANIA NYONGEZA YA POSHO ZA VIONGOZI WA CCM

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Albert Chalamila ameonekana kutoridhishwa na kiwango cha posho wanazolipwa viongozi wa chama hicho wakati wakihudhuria vikao mbalimbali na kuagiza watendaji kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya vikao hivyo.

Katika ziara yake ya kwanza tangu achaguliwe kushika wadhifa huo mwishoni mwa mwaka jana aliyofanya wiki iliyopita katika wilaya za kichama za Mufindi, Iringa Vijijini na Iringa Manispaa, Chalamila alijikuta akilazimika kutoa fedha yake ya mfukoni kuchangia posho za wajumbe wa halmashauri kuu za CCM wa wilaya hizo.

Alipokutana na halmashauri ya CCM wilaya ya Mufindi, Chalamila alichangia Sh Milioni 2.5 kwa wajumbe wa kikao hicho ikiwa ni nyongeza ya Sh 15,000 kwa kila mjumbe baada ya Katibu wa wilaya hiyo Elirehema Nassar  kutoa taarifa kwamba wangelipwa kati ya Sh 10,000 na 30,000 kutegemea na umbali wanaotoka.

Akiwa Iringa Vijijini mwenyekiti huyo aliyekuwa pia Mjumbe wa Kamati ya Kuhakiki Mali za Chama iliyoundwa mapema mwaka huu na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk John Magufuli alichangia Sh Milioni 2.3 ikiwa ni nyongeza ya Sh 15,000 kwa kila mjumbe baada ya Katibu wa CCM wa Iringa Vijijini, Dodo Sambu kusema walipanga kuwalipa nauli ya Sh 10,000 kila mmoja kutokana na ufinyu wa bajeti.

Juzi Jumamosi, Chalamila alikutana na halmashauri ya CCM ya Manispaa ya Iringa na kuchangia Sh Milioni 1.5 ikiwa ni nyongeza ya Sh 20,000 kwa kila mjumbe baada ya Katibu wa CCM wa manispaa hiyo, Marko Mbanga kutoa taarifa kwamba stahiki ya wajumbe wa kikao hicho ni nauli ya Sh 5,000 kwa kila mmoja.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wajumbe wa vikao hivyo, mwenyekiti huyo alisema angependa kuona wajumbe wa vikao hivyo nyeti wanaofanya kazi kubwa ya kukijenga chama hicho kwa kujitolea wanalipwa posho inayolingana na hadhi yao.

“Nitafurahi nikiona wajumbe wanalipwa hata zaidi ya Sh 100,000 kwa kila kikao wanachohudhuria kutokana na hadhi yao,” alisema.

Alisema katika maeneo mengi ya mkoa wa Iringa, CCM ina miradi mingi iliyoendelezwa, iliyo katika hatua ya kuendelezwa na inayotakiwa kuendelezwa ambayo kama itasimamiwa vizuri inaweza kukiwezesha chama hicho kuboresha posho na maslai ya viongozi na watumishi wake.

Akitoa mfano wa baadhi ya mali za chama hicho zilivyokuwa zikitumika vibaya, Chalamila alisema, wafanyabishara waliopanga katika maghala yaliyopo katika uwanja wa Samora walikuwa wakilipa kiasi kidogo sana cha fedha kwa mwezi kabla mikata hiyo haijarekebishwa.

“Wafanyabiashara hao walikuwa wakilipa fedha ndogo sana kwa kisingizio kwamba maghala hayo walijenga wao wenyewe. Nikasema hii haikubaliki na ni bora waondoke au tubomoe maghala hayo,” alisema.

Katika kupunguza mianya ya upotevu wa fedha za chama hicho, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Christopher Magala alisema chama hicho kimepiga marufu wapangaji wake kupangisha majengo yake wapangaji wengine.

“Tunaendelea kufuatilia na kuwatambua wote waliopangishwa majengo ya CCM na watu baki ili wawe wapangaji wetu halali, hatutaki biashara ya mtu kati kwani biashara hii imekuwa ikiwanufaisha watu baki badala ya chama; mpangaji wetu ni lazima awe yule mwenye mkataba na chama na si vinginevyo,” alisema.

Aidha alisema mwa CCM yoyote atakayebainika kutumia kwa maslai yake binafsi mali za chama hicho au kutafuna fedha za chama kinyume na taratibu atafikishwa katika vyombo vya dola na kushitakiwa kama mwizi mwingine yoyote.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment