Sunday, 10 June 2018

CHALAMILA AKABIDHI MIPIRA 75 KWA MATAWI YA CCM IRINGA MJINI

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Albert Chalamila ametoa mipira 75 kwa ajili ya matawi 75 ya chama hicho Iringa Mjini itakayotumika kuanzisha timu na ligi itakayotumiwa kuhamasisha michezo na shughuli za chama hicho.

Mipara hiyo ya kisasa iliyonunuliwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas ilikabidhiwa jana kwa mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa, Said Rubeya katika hafla fupi iliyohudhuriwa pia na baadhi ya wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya Manispaa hiyo.

Pamoja na mipira hiyo ya awali, Asas ameahidi kutoa seti moja ya jezi na mpira mwingine mmoja mmoja kwa timu za matawi hayo ili kuziwezesha kujiandaa vizuri na mashindano hayo.

“Ligi hiyo itakuwa sehemu ya mkakati wa chama chetu kutangaza utekelezaji wa Ilani na kuhamasisha wanachama kujiandaa na chaguzi mbalimbali zijazo,” alisema Chalamila.

Pamoja na mkakati huo alisema CCM inatambua umuhimu wa michezo kwa afya za watanzania na chanzo kizuri cha ajira.

“Hakuna asiyejua jinsi michezo inavyolipa. Kuna mabadiliko makubwa katika michezo hasa wa soka nchini na hamasa imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kwani mchezo huo unalipa kuliko kazi nyingi,” alisema huku akitoa mfano wa mishahara mikubwa ya baadhi ya wachezaji wa ndani na nje ya nchi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment