Thursday, 14 June 2018

ASAS KULETA LIGI KUBWA YA MPIRA WA MIGUU MKOANI IRINGAMKOA wa Iringa unatarajia kuingia katika ligi ya mpira wa miguu kubwa kuliko zote zilizowahi kutokea; baada ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Salim Asas kutangaza kumwaga vifaa mbalimbali vya michezo kwa matawi yote 549 ya chama hicho.

Vifaa hivyo ambavyo thamani yake haikuwekwa bayana japokuwa vinaelezwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh Milioni 150 vinajumuisha mipira na jezi  zitakazotolewa kwa timu 549 za matawi hayo.

Akitoa taarifa hiyo kwa wajumbe wa halmahauri kuu za CCM za wilaya zote za mkoa wa Iringa katika ziara yake aliyofanya katika wilaya hizo hivikaribuni, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Albert Chalamila alisema vifaa hivyo vya kisasa vimeagizwa toka nje ya nchi.

“Najua thamani ya mpira mmoja ni Sh 120,000 na seti moja ya jezi Sh 200,000, kwahiyo zote zinaweza kuwa zimegharimu zaidi ya Sh Milioni 150,” alisema.

Alisema wakati matawi hayo yakisubiri kugaiwa vifaa hivyo wanatarajia taratibu za kuunda timu za vijana katika kila tawi zitaanza kuunda ili zishiriki ligi kubwa itakayopigwa kwa ngazi ya matawi, kata, wilaya na hadi mkoa.

“Tunataka kila mahali uchezwe mpira wa miguu na kwa kufanya hivyo tutakuwa tunachangia juhudi za serikali za kuinua mchezo wa soka nchini kama ilivyofafanuliwa katika Ilani yetu,” alisema.

Kwa kupitia mpango huo, Chalamila alisema kila tawi litapa mpira mmoja na seti moja ya jezi, vifaa vitakavyowawezesha kushiriki katika ligi hiyo.

Wakati huo huo Chalamila alisema matawi 75 ya chama hicho Iringa Mjini yamekwishapewa mpira mmoja mmoja na kwa upendeleo yatapewa tena mipira hiyo na jezi baada ya taratibu kukamilika.

“Jicho la CCM lipo Iringa Mjini, na jimbo hilo linaongozwa na Chadema, kwahiyo ni muhimu tukawapa upendeleo kwa manufaa ya chama,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment