Friday, 8 June 2018

ALIYEMUHONGA AFISA WA SUMATRA IRINGA AHUKUMIWA JELA MIAKA 3, ALIPA FAINI

Image result for mahakama

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Iringa imemtia hatiana na kumuhukumu Emmanuel Mwipopo (41) mkazi wa Kihesa mjini Iringa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kutoa hongo kinyume na kifungu cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Mwipopo alifikishwa katika mahakama hiyo akituhumiwa kumuhonga Sh 100,000 Afisa Mfawidhi wa Sumatra mkoa wa Iringa, Patel Ngereza ili abadilishiwe njia ya gari lake la kusafirishia abiria maarufu kama daladala.

Alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Agosti 9, 2017 na kusomewa shtaka hilo na mwendesha mashtaka wa Takukuru , Elisante Fundisha.

Akisoma hukumu ya shauri hilo hivikaribuni, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, David Ngunyale alisema mahakama imetoa adhabu hiyo baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa kati ya Februari na Machi mwaka 2017 mshtakiwa akiwa wakala wa gari ya biashara lenye namba T546 DFT Toyota Hiace mali ya Saul Malogo alimshawishi na kumuhonga jumla ya Sh 100,000 aliyekuwa Meneja wa Sumatra mkoani Iringa ili abadilishiwe njia.

Kwa kutumia simu yake ya mkononi, Machi 2, 2017 Mwipopo alituma kwa afisa huyo wa Sumatra kiasi hicho cha fedha kwa kupitia wakala wa M-Pesa ili kutimiza azma yake ya kumshwishi kubadilisha gari njia ya gari hilo.

Mwipopo alitaka gari hiyo iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Barabara Mbili na Viwengi, iwe inafanya safari kati ya Stendi Kuu na Chapuya.

Alikamatwa na kufikishwa mahakamani hapo baada ya Takukuru kupokea taarifa hiyo.

Kufuatia hukumu hiyo,  Mwipopo alilipa faini hatua iliyomuwezesha kukwepa kifungo cha miaka mitatu jela.

Akizungumza na wanahabari baada ya hukumu hiyo, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Aidan Ndomba ametoa wito kwa wakazi wote kutofumbia macho rushwa kwa kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ili iwezi kuchukua hatua za haraka

Reactions:

0 comments:

Post a Comment