Wednesday, 23 May 2018

ZAWADI RITTA KABATI CUP ZAPAA, LIPULI FC YAKARIBISHWAPAZIA la mashindano ya ligi ya mpira wa miguu ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati (Ritta Kabati Challenge Cup 2018) limefunguliwa huku zawadi zike zikielezwa zikikwea zaidi ya mwaka jana.

Akizungumza na wanahabari mwenyekiti wa mashindano hayo Gerald Malekela alisema wanazialika timu mbalimbali za mkoa wa Iringa ikiwemo timu ya Lipuli inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kuchukua fomu za ushiriki wa mashindano hayo pendwa.

“Dirisha la uchukuaji fomu lilifunguliwa Mei 21 na litafungwa Mei 31 kabla ya mashindano hayo yatakayopigwa kwa takribani mwezi mmoja kwa njia ya mtoano kuanza rasmi Juni 10,” alisema.

Malekala alisema gharama ya fomu ya ushiriki imepanda kutoka Sh 20,000 za mwaka jana hadi Sh 30,000 mwaka huu hiyo ikitokana na ongezeko la gharama zake za uendeshaji.

Alisema fomu hizo zinapatika katika kituo cha redio cha Nuru FM na vituo vingine vyote vya redio za mjini Iringa.

Wakati bingwa wa mashindano hayo wa mwaka jana aliondoka na kombe, pikipiki aina ya SUNLG na cheti, Malekela alisema bingwa wa mwaka huu ataondoka na fedha taslimu Sh Milioni mbili, kombe lenye thamani ya Sh Milioni moja na cheti.

Alisema wakati mshindi wa pili wa mwaka jana aliondoka na Sh 500,000 wa mwaka huu ataondoka na Sh Milioni moja huku mshindi wa tatu akitarajiwa kujiwekea kibondoni Sh 500,000 kutoka Sh 200,000 za mwaka jana.

Alisema kutakuwa pia na zawadi za kati ya Sh 100,000 na Sh 200,000 kwa wachezaji, waamuzi na washangiliaji bora wa mashindano hayo.

Akizungumzia malengo la ligi hiyo Katibu wa Kamati ya Mashindano hayo, Fred Mgunda alisema ni pamoja na kuibua vipaji vya vijana mkoani Iringa, kuonesha uwezo wa vijana na kutengeneza ajira kwao na kujenga kizazi chenye afya bora na kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi.

Mengine ni kutoa burudani kwa wakazi wa Iringa, kuwakutanisha vijana pamoja ili kuzungumza lugha moja ya kimichezo na maendeleo, kuwaepusha vijana na makundi au vijiwe visivyofaa, kuhamasisha michezo katika mkoa wa Iringa na kutimiza agizo la makamu wa Rais juu ya kufanya mazoezi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment