Wednesday, 16 May 2018

NAPE, BASHE WAOMBA WABUNGE WAIKATAE BAJETI YA KILIMO


Image result for bashe bungeni


WAKATI Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ameitaka Serikali kutoona aibu kuiondoa bungeni bajeti ya Wizara ya Wizara ya Kilimo ili ikajipange upya kwa maelezo kuwa bajeti hiyo itaiumiza Serikali ya Awamu ya Tano, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amewataka wabunge wenzake kuungana na kuikataa bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2018/19 ili kuipa nafasi Serikali kuwasilisha bungeni bajeti itakayogusa maisha ya Watanzania.

Nape  na Bashe wametoa kauli hizo leo Jumatano Mei 16, 2018 wakati wakizungumza katika mjadala wa bajeti hiyo bungeni mjini Dodoma.

Waziri huyo wa zamani wa habari amesema umefika wakati wa kueleza ukweli kuwa bajeti ya wizara hiyo ni ngumu na haiendani kabisa la Ilani ya uchaguzi ya CCM, ikipitishwa itakuwa mwiba kwa Serikali.

Bashe amewaomba wabunge watumie kanuni ya 69 ya Bunge kuirudisha Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha zikaketi ili kuja na bajeti inayogusa maisha ya watu.

Amesema haiwezekani sekta inayogusa asilimia 70 ya Watanzania na kuchangia asilimia 30 katika pato la Taifa ikatengewa asilimia 0.8 ya fedha za maendeleo katika bajeti kuu ya Serikali.

“Sekta hii imeendelea kuonewa kwa muda mrefu na siyo sahihi, hasa wabunge wa CCM tuna wajibu wa kumlinda mkulima,” amesema Bashe.

Naye Nape amesema Bajeti hii inagusa maisha ya watu hivyo ujumbe unaotakiwa kwa wananchi ni je, Serikali inajali maendeleo ya vitu au watu waliowaweka madarakani jambo ambalo majibu yake yatakuwa na maana tofauti kwa wananchi.”

Amesema anamuonea huruma Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba kwa maelezo kuwa kuna mambo yaliyo nje ya uwezo wake, lakini kila jambo anabebeshwa yeye. “Ni mtihani mkubwa kwa Serikali katika bajeti ambayo inagusa asimilia 80 ya Watanzania.

“Wakati fulani tulisema Serikali ikwepe kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi mikubwa inayoweza kujiendesha kibiashara, lakini tukashambuliwa kama si wazalendo katika nchi hii, na hili Tizeba tutakubebesha bure lakini si lako,” amesema Nape.

Amesema akikubali bajeti hiyo, wananchi wake wa Mtama na wakulima wa korosho, ufuta, pamba na mazao mengine nchini watamshangaa kwa kiasi kikubwa hivyo hakuna shida wala aibu kukaa pamoja na kuifumua kama ilivyowahi kufanyika kwa wizara nyingine.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment