Monday, 21 May 2018

MWENGE WA UHURU KUHIMIZA MAPAMBANO YA UKIMWI IRINGA


MKOA wa Iringa umejipanga kikamilifu kutumia mbio za Mwenge Uhuru kuhimiza mapambano dhidi ya Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Hatua hiyo inajibu ombi la Rais Dk John Magufuli ambaye hivi karibuni aliutaka mkoa huo kuongeza mapambano dhidi ya maambukizi hayo kwa kigezo kwamba takwimu zake zinaongezeka wakati za kitaifa zinashuka.

Matokeo yanayotokana na utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi Tanzania (THIS) ya mwaka 2016/2017 yanaonesha maambukizi katika mkoa wa Njombe unaoongoza kitaifa yamepungua kutoka asilimia 14.8 mwaka 2011/2012 hadi asilimia 11.4 na mkoa wa Iringa ambao ni pili yameongezeka kutoka asilimia 9.1 hadi asilimia 11.3.

Akizungumza na wahabari leo wakati akitoa taarifa ya ujio wa mwenge mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema mapmbano dhidi ya maambukizi hayo yanakwenda na kauli mbiu isemayo “mwananchi jitambue, pima afya yako sasa.”

Masenza alisema pamoja na kampeni hiyo, mwenge huo utatoa ujumbe maalumu wa mapambano dhidi ya maralia, dawa za kulevya na rushwa, na utatilia mkazo umuhimu wa uwekezaji katika elimu unaofanywa na serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa maendeleo.

Alitaja shughuli zingine zitakazofanywa na mbio hizo za mwenge kuwa ni pamoja na kukagua miradi 40 ya maendeleo  yenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 24.4 katika sekta ya elimu, afya, maji, maliasilia, kilimo, viwanda na uvuvi.

Alisema mkoa wa Iringa utaanza mbio za Mwenge Mei 23 hadi Mei 27 baada ya kuupokea kutoka mkoa wa Mbeya na ukiwa mkoani humo utapita katika halmashauri zote tano kutoa ujumbe huo na kuhimiza maendeleo.

Alisema Mwenge huo utaanza kukimbizwa katika halmashauri ya Mufindi, Mei 23 na Mei 24 utaelekea halmashauri ya wilaya ya Iringa, Mei25 utakuwa halmashauri ya wilaya ya Kilolo, Mei 26 halmashauri ya manispaa ya Iringa na Mei 27 utakimbizwa katika halmashauri ya Mji Mafinga.

Baada ya kukimbizwa katika mkoa wa Iringa, alisema Mwenge huo utakabidhiwa kwa mkoa wa Njombe

Reactions:

0 comments:

Post a Comment