Tuesday, 8 May 2018

MHANDISI MSHANA AKAMATWA KASHFA YA UJENZI CHUO KIKUU MKWAWAJESHI la Polisi mkoa wa Iringa limemkamata Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya MNM Engineering Service Ltd, Mhandisi Godwin Mshana kwa tuhuma ya kujenga chini ya kiwango, ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Mkwawa (MUCE) cha mjini Iringa.

Kukamatwa kwa Mhandisi Mshana ni utekelezaji wa agizo lililotolewa hivikaribuni chuoni hapo na Rais Dk John Magufuli la kufuatilia madai ya kuwepo kwa ubadhilifu wa fedha katika ujenzi wa ukumbi huo liogharimu Sh Bilioni 8.

Akizungumza na wanahabari jana jioni, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alisema Mhandisi Mshana ambaye ni mkandarasi maarufu wa mjini Iringa alikamatwa akiwa nyumbani kwake Mei 3 ikiwa ni siku moja baada ya Rais kutoa agizo hilo.

“Baada ya kumkamata mkandarasi huyo tumeunda kikosi kazi kinachojumuisha Takukuru  ili kwa pamoja tufanye uchunguzi wa kina wa tukio hili,” alisema bila kuzungumzia hatma ya dhamana ya mtuhumiwa huyo kwasasa.

Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Iringa Aidan Ndomba alisema baada ya mkandarasi huyo kukamatwa kikosi kazi chao kinaendelea na uchunguzi wa ujenzi huo ambao thamani yake inaonekana kuwa juu zaidi ya thamani halisi ya jengo.

Alisema mkandarasi huyo alifanya kazi hiyo kwa miaka minne na nusu kwa Sh Bilioni 3.6 bila kumaliza ujenzi huo ambao baadaye uliendelezwa na mkandarasi mwingine na kufanya thamani yake ifike Sh Bilioni 8.8.

“Kwahiyo huu ni uchunguzi mkubwa kwasababu unahusu fedha nyingi. Watu wengi wanaweza kuhusishwa na kashfa hii katika awamu ya kwanza na ya pili ya ujenzi wake,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment