Sunday, 6 May 2018

MBUNGE ROSE TWEVE AVIMWAGIA MAHELA VIKUNDI VYA UWT, ASAS AMUUNGA MKONO

Image result for rose tweve


MBUNGE   wa Viti Maalum  Mkoa  wa  Iringa Rose Tweve (CCM) ametoa Sh Milioni 27 kwa vikundi  45  vya Kuweka na Kukopa (Vicoba) mkoani Iringa watakazokopeshana ili kuinua mitaji ya shughuli zao za ujasiriamali.

Vikundi hivyo vilivyopo katika majimbo mbalimbali ya mkoa wa Iringa vinaundwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)  wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumzia  azma yake ya kuwawezesha wanawake wa umoja huo, Mbunge Tweve alisema kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya Sh Milioni 60 alizoahidi kwa vikundi hivyo vya wanawake katika kata zote 107 za mkoa wa Iringa.

“Fedha nazotoa kwa vikundi hivyo zinatoka katika mshahara wangu kama mbunge ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya kusaidia kuwainua kiuchumi akinamama wa UWT niliyotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alisema.

Alisema  baadhi ya vikundi vilivyoanza kunufaika na utekelezaji wa ahadi hiyo ni pamona na vile vilivyopo katika majimbo ya wilaya ya Mufindi, Kilolo, Isimani na Kalenga.

Alisema mafanikio ya utekelezaji wa mpango huo yamemvutia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas ambaye kwa kuunga mkono juhudi hizo ameahidi kuchangia Sh Milioni 53 kwa kata zote za mkoa wa Iringa kwa kupitia Mfuko wa Mbunge Rose Tweve.

“Kazi nzuri tunayoendelea kuifanya kwa wanawake wa UWT katika kata za mkoa wa Iringa imemvutia MNEC, na atachangia kiasi kikubwa cha fedha katika mfuko wa mbunge ili tuendelee kuwawezesha wanawake wengi zaidi wakiwemo pia wale ambao sio wa CCM,” alisema.

Kwa kupitia mpango huo wa kuwawezesha kiuchumi wa wanawake wa UWT katika kata hizo, Tweve alisema amekuwa akichangia Sh 600,000 kwa kila kikundi na kwa vikundi vinavyofanya vizuri vimekuwa vikipewa tuzo ya Sh 400,000.

“Mfano ni kikundi cha Nzihi, Iringa Vijijini ambacho kwasasa kina mtaji wa zaidi ya Sh Milioni nane baada ya kuchangiwa Sh 600,000 kupitia mfuko wangu wa mbunge,” alisema na kuongeza kwamba kikundi hicho tayari kimepewa tuzo hiyo ya Sh 400,000.

Pamoja na mafanikio hayo Tweve alisikitika akisema kikundi cha kata ya Ulanda kimeshindwa kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na badala yake baadhi ya viongozi wake wanatuhumiwa kuzitumia kwa mambo yao binafsi.

“Kikundi kama hicho kiarudisha nyuma jitihada hizi na kwa kweli kuna haja ya kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwataka waliohusika warejeshe fedha hizo katika kikundi,” alisema.

Katibu  wa  UWT  Iringa Vjijini, Asha Stambuli alisema jumuiya yao haitasita kuwachukulia hatua kali viongozi watakaohusika na matumizi mabaya ya fedha hizo akisisitiza “fedha hizo sio sadaja ni fedha zinazopaswa kuleta maendeleo kwa wanawake na ndani ya jumuiya.”

Akipongneza juhudi za mbunge huyo, Mwenyekiti  wa UWT  Iringa  vijijini, Lenah Hongole alisema UWT inao mpango wa kuwa na taasisi yake ya kifedha ili kuunga juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali katika kuwainua kiuchumi wanawake na jumuiya hiyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment