Wednesday, 30 May 2018

KITUO CHA KUUZIA BIDHAA ZA ASILI NA UTAMADUNI CHAZINDULIWA IRINGA VIJIJINI

MRADI wa Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST) umetumia zaidi ya Sh Milioni 46 kujenga kituo cha kuuzia bidhaa za asili na utamaduni pembezoni mwa barabara inayolekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika kijiji cha Malizanga, Iringa Vijijini.

Kituo hicho kinatarajia kuwanufaisha akina mama wa kimasai zaidi ya 20 wanaounda kikundi cha NAMAYANA ambao awali walikuwa wakiuza bidhaa hizo katika mazingira yasio rafiki na watalii; chini ya ardhi na juu ya meza za miti iliyosimikwa ardhini.

Uzinduzi wa kituo hicho ulifanywa juzi na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Getrude Lyatuu katika hafla iliyohudhuriwa na akinamama hao, wazee wa kimila na viongozi mbalimbali wa halmashauri ya wilaya ya Iringa na Mkoa wa Iringa.

UNDP kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa Mzingira (GEF) ndio waliokuwa wafadhili wakuu wa mradi wa SPANEST unaokwenda ukingoni baada ya kutekelezwa katika maeneo yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania kwa zaidi ya miaka mitano.

Akizindua kituo hicho, Lyatuu ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Mazingira wa UNDP alisema; “Ni matumaini yangu kwamba kituo hiki kitakuwa chachu ya mabadiliko ya maisha yenu, hatutarajii kuona hali zenu zinazodi kuwa duni baada ya kituo hiki kuja.”

Lyatuu aliwataka akina mama hao kutumia sehemu ya faida wanayopata katika biashara yao kuboresha huduma na bidhaa wanazotengeneza na kuwapeleka shule vijana wao ili wakajifunze lugha mbalimbali hatua itakayosaidia kurahisisha mawasiliano na watalii kutoka nchi mbalimbali wanaotembelea hifadhi ya Ruaha.

Awali Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Maing’ataki alizungumzia ujenzi wa kituo hicho akisema umejumuisha banda la kuuzia bidhaa hizo pamoja na stoo yake, banda la kupumzikia, vyoo vya kisasa na huduma ya maji ya bomba.

Meing’ataki alisema kabla ya ujenzi huo, mradi uliwawezesha viongozi wa kikundi hicho kufanya ziara ya mafunzo katika mikoa ya Arusha na Manyara walikojifunza namna ya kuziongezea ubora bidhaa za utamaduni, jinsi ya kupokea wageni na kuwahudumia kwa usafi.

Katika risala yao iliyosomwa na Maria Singai, akinamama hao wa NAMAYANA walisema kabla ya kituo hicho walikuwa wakipanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara na kuathiriwa na jua kali, vumbi na mvua.

Afisa Utalii wa HIfadhi ya Taifa ya Ruaha, Tulidanga George alisema aliwataka wana Malizanga kutumia fursa ya kituo hicho na ahadi ya serikali ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Iringa mjini hadi katika hifadhi hiyo kujifunza historia na tamaduni zao, lugha mbalimbali na namna kuongoza watalii.

Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho, Lulamo Kadaga alitoa ombi kwa wadau kuwasaidia kujenga hoteli katika kituo hicho ili huduma za chakula na malazi zipatikane kwa wageni wanaotaka kupumzika huku akitaka kitangazwe kimataifa hatua itakayowawezesha watalii kukifahamu hata kabla ya kukitembelea.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment