Wednesday, 16 May 2018

HAKIMU ANAYESIKILIZA KESI YA ABDUL NONDO AGOMA KUJITOAHAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, John Mpitanjia leo amegoma kujitoa kusikiliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP) Abdul Nondo anayeshitakiwa mahakamni hapo kwa makosa mawili.

Nondo ameshitakiwa kwa kuchapisha taarifa za uongo kwamba yupo hatarini na kuzisambaza mtandaoni na kutoa taarifa za uongo kwa askari Polisi Koplo Salim wa Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kupelekwa kiwanda cha Pareto Mafinga.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 13 ya mwaka 2018 ilidaiwa kwamba Machi 7, mwaka huu akiwa Ubungo jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alitenda kosa la kuchapisha taarifa hizo akitumia simu ya kiganjani yenye No. 0659366125 kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao na kusambaza katika mitandao ya kijamii.

Juzi, mshatakiwa huyo aliandika barua ya kumkataa hakimu huyo kwa kile alichosema amekuwa na mawasiliano na baadhi ya mashahidi wa upande wa Jamuhuri jambo linalomkosesha imani ya kutendewa haki.

Akitoa uamuzi huo mdogo jana, Hakimu Mpitanjia alisema kuwa  sababu alizotoa mshtakiwa hazina msingi wowote na ataendelea kusikiliza shauri hilo ili pande zinazohusika zisichelewe kupata haki.

“Sababu walizotoa upande wa utetezi ni za kufikirika ambazo hazina ushahidi wowote na kwa kuwa mahakama ni chombo cha mwisho katika kutenda haki na kuwahisha haki, nitaendelea kusikiliza shauri hili kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Akizungumzia uamuzi huo wa mahakama, Wakili wa Nondo, Jebra Kambole alisema upande wa utetezi umepokea uamuzi huo wa mahakama na hauna haja ya kuupinga  na sasa wamejielekeza kutumia njia nyingine za kisheria kupata haki yao.

“Kwa sasa tunaona shauri hili liendelee tu tutapambana mahakamani ili mteja wetu aweze kupata haki yake,” alisema.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 18 ambapo upande wa Jamuhuri unategemea kulita mashahidi wake wawili watakaotoa ushahidi dhidi ya shauri hilo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment