Wednesday, 16 May 2018

DC AWAPA SIKU 7 WADAIWA SUGU WA SIDO IRINGA KUFANYA MAREJESHO


MKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela leo ametoa siku saba kwa wadaiwa sugu 891 wanaodaiwa zaidi ya Sh Milioni 293 na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Iringa kulipa mikopo yao.

Akizungumza na wanahabari jana mbele ya maafisa wa shirika hilo, alisema baada ya siku saba kwisha, serikali itachukua hatua stahiki ikiwa ni kupita nyumba kwa nyumba kwa kila mkopaji na wadhamini wao na kuchukua hatua stahiki.

Kasesela alisema ofisi yake imeamua kushirikiana na SIDO kudai mikopo hiyo kwa kuzingatia kwamba shirika hilo ni la umma lisilotakiwa kukwamisha ili fursa ifike kwa watu wengine zaidi.

“Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Meneja wa SIDO Mkoa wa Ireinga, serikali imebaini kuwepo kwa wadaiwa sugu wa mikopo waliolimbikiza fedha nyingi jambo linalowanyima fursa wajasiriamali wengine kukopa,” alisema.

Alisema SIDO inategemewa sana kusukuma uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vidogo kupitia huduma hii ya utoaji wa mikopo ili kuwanufaisha watanzania  kwahiyo haistahili kuwavumilia watu wanaoikwamisha.

“Nawaagiza wakopaji wote popote walipo mkoani Iringa au wamehama mkoa wajue kuwa kumbukumbu za madeni yao zipo, picha zao zipo, majina yao yapo na wadhamini wao wapo, hivyo wanatakiwa kulipa mikopo hiyo” alisema.

Meneja wa SIDO mkoa wa Iringa Francisca Simoni alisema SIDO pamoja na huduma zingine zinazotolewa inatoa ushauri wa fedha na mikopo inayolenga kukuza biashara na viwanda vidogo vinavyoanzishwa au vilivyoanzishwa tayari lakini vinahitaji mikopo ili kukua.

Alisema kati ya wadaiwa hao 293, wadaiwa 167 ni binafsi wanaodaiwa jumla ya Sh 181, 396,500 na vikundi 15 vyenye wanachama 721 vinavyodaiwa jumla ya Sh 111,984,425.

Simoni alisema sehemu kubwa ya wadaiwa hao wapo mjini Iringa wakidaiwa jumla ya  Sh 269,331, 225 na kiasi kinachobaki kinadaiwa katika wilaya zingine za mkoa wa Iringa zikiwemo Sh 4,858,700 zinazodaiwa Iringa Vijijini.

Awali Afisa Mikopo wa SIDO, Neserian Laizer alisema malimbikizo hayo ya kati ya mwaka 2014 hadi sasa yamelizuia shirika kuendelea kutoa huduma hiyo ya mikopo hiyo ambayo ni kati ya Sh 100,000 na Sh 500,000 kwa mkopaji mmoja.

Naye Afisa Biashara wa SIDO, Niko Mahinya alisema SIDO imeamua kuunganisha nguvu na serikali kudai mikopo hiyo baada ya juhudi zake kukwamishwa na taasisi zingine wakiwemo madalali waliopewa kazi hiyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment