Monday, 14 May 2018

ABDUL NONDO AMKATAA HAKIMU ANAYESIKILIZA KESI YAKE
MWENYEKITI wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP) Abdul Nondo anayeshitakiwa katika mahakama ya hakimu mkazi Iringa ameandika barua ya kumkataa hakimu mkazi wa mahakama hiyo John Mpitanjia kuendelea kusikiliza kesi yake akisema ana viashiria vya kutomtendea haki.

Nondo ameshitakiwa kwa makosa mawili ya kuchapisha taarifa za uongo kwamba yupo hatarini na kuzisambaza mtandaoni na kutoa taarifa za uongo kwa askari Polisi Koplo Salim wa Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kupelekwa kiwanda cha Pareto Mafinga.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 13 ya mwaka 2018 ilidaiwa kwamba Machi 7, mwaka huu akiwa Ubungo jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alitenda kosa la kuchapisha taarifa hizo akitumia simu ya kiganjani yenye No. 0659366125 kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao na kusambaza katika mitandao ya kijamii.

Hakimu Mpitanjia leo alilazimika kuahirisha kuendelea kusikiliza ushahidi uliokuwa utolewa na mashahidi wawili wa upande wa mashitaka ili kupata msimamo wa mawakili wa pande zote mbili, Jamuhuri na utetezi juu ya sababu zilizotolewa na Nondo zikimtaka ajiondoe kusikiliza kesi hiyo.

Wakili wa utetezi, Jebra Kambole alisema anakubaliana na sababu tano zilizotolewa na mteja wake akiomba hakimu huyo ajitoe kusikiliza kesi hiyo ili mahakama hiyo iweze kutenda haki kwa pande zote mbili.

Moja ya sababu zilizoelezwa mahakamani hapo ni  pamoja na ujirani na mawasiliano anayodaiwa kuwa nayo hakimu huyo na Shahidi wa Jamuhuri, Kamanda wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa, RCO Kasindo kila kesi hiyo inapofikishwa mahakamani hapo.

Ukitoa mfano, upande huo wa utetezi ulisema mahakamani hapo kwamba April 15, 2018 hakimu huyo alionekana akiondoka katika eneo la mahakama hiyo akiwa na RCO huyo kwa kutumia gari la kiongozi huyo wa Polisi ambaye ofisi yake ndiyo iliyofanya uchunguzi wa kesi yake jambo linalompa hofu ya haki kutendeka.

Ukipinga hakimu huyo kujitoa upande wa Jamuhuri ukiongozwa na wakili Abel Mwandalama anayesaidiwa na Alex Mwita ulikiri kupokea nakala ya barua ya malalamiko ya Nondo lakini ukapinga sababu zilizotolewa kwa madai kwamba zinakosa msingi kwasababu zimetolewa bila ushahidi wowote.

“Hakuna ushahidi wowote katika sababu zake hizo za malalamiko zinazoweza kuifanya mahakama au wewe mwenyewe ujiondoe kusikiliza kesi hii, ni malalamiko dhaifu yasio na ushahidi” alisema.

Baada ya kusikiliza maoni ya pande hizo mbili, Hakimu Mpitanjia aliahirisha shauri hilo mpaka keshokutwa Mei 16 atakapotoa uamuzi mdogo kama aendelee au asiendelee kusikiliza kesi hiyo.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya maamuzi hayo, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu Tanzania (THRD), Onesmo Ole Ngurumo alisema ni haki ya mtuhumiwa kumkataa hakimu baada ya kujiridhisha kwamba mwenendo wake unaweza kusababisha haki isitendeke kwa pande zote.

“Kama watetezi wa haki za binadamu, ombi letu tunaomba mahakama impe hakimu anayeweza kuwa katikati katika maamuzi. Awe kama mwamuzi wa mpira asiegemee upande fulani,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment