Thursday, 5 April 2018

WAZEE IRINGA WAHOFIA NDUGU KUOANA, WAKE KUTUMIA MAJINA YA WAUMEWAZEE wa kimila wa mkoani Iringa wameeleza kujawa na hofu ya uwezekano wa wanafamilia wa koo moja kuoana wao kwa wao kwa kile walichadai ni kwasababu ya mmomonyoko wa mila, desturi na tamaduni za makabila mbalimbali nchini.

Wakizungumza na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Dk Harrison Mwakyembe hivikaribuni mjini Iringa, wazee hao walisema pamoja na mmomonyoko huko, idadi ya watanzania wasioweza kuzungumza lugha zao za asili (makabila) inapungua siku hadi siku.

Mmoja wa wazee hao, Evaristo Mgata alisema watanzania walio wengi, hasa wanaoishi mijini wanazidi kuonesha bidii ya kujifunza tamaduni za Ulaya tofauti na za kwao wakiamini kwa kufanya hivyo wanapiga hatua muhimu zaidi kimaisha.

“Hali hii imewafanya baadhi yao wasijue mila, tamaduni na desturi za makabila yao  hatua inayowafanya washindwe pia kuzungumza lugha za makabila yao," alisema

Alisema jambo hilo lisipotafutiwa ufumbuzi na kuachwa likomae miongoni mwa jamii, siku si nyingi kutakuwa na Taifa la watu wasiojua wapi wanatokana na wapi wanakwenda.

Akizungumzia uwezekano wa wanafamilia wa ukoo mmoja kuoana tofauti na mila na tamaduni zao, Mgata alisema mbali na mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea mijini, hali hiyo inachochewa na namna familia za sasa zinavyotumia majina yake.

“Watanzania walio wengi wanatumia majina mawili, jina lake na la baba, wachache wanatumia majina ya ukoo. Katika mazingira ya koo zisizoishi mahali pamoja sio rahisi kujuana kama ni ndugu wa ukoo mmoja jambo linaloongeza hatari hiyo,” alisema.

Mgata alihoji pia sababu za baadhi ya wake kutumia majina ya waume zao akisema hali hiyo imekuwa ikileta mkanganyiko kwa baadhi ya koo.

Akitoa mfano alisema; “Mimi ni mhehe, nimeishi Mwanza kwa miaka mingi. Nilipostaafu na kurudi kijijini Iringa, kuna siku tulipata wageni, wakati wa utambulisho mke wangu akasema yeye ni Mama Mgata. Maelezo yake yakawachanga wageni na kuniuliza sababu za kuoa dada yangu kwasababu mimi pia ni Mgata.”

Katika jitihada zao za kushughulikia mila, desturi na tamaduni za watu wa mkoa wa Iringa wazee hao walisema wameunda umoja ambao pamoja na jambo hilo nyeti umepanga kujenga kituo kikubwa cha mila mjini Iringa.

Mwenyekiti wa umoja huo, Augustino Stambuli aliiomba serikali iwasaidie kupata eneo na fedha za kuwawezesha kutimiza lengo hilo.

“Mbali na simulizi za mila, tamaduni na desturi za watu wa mkoa wa Iringa katika jengo hilo kutakuwa na zana na vitu mbalimbali vya kale vilivyotumiwa na makabila ya watu wa Iringa,” alisema.

Pamoja na mipango hiyo aliiomba serikali iwape vipindi, hasa katika shule za msingi, ili waweze kufundisha na kuwakumbusha wanafunzi umuhimu wa kujua mila na tamaduni zao.

Akizungumzia umuhimu wa watanzania kutumia majina yao yote ili kutambulisha koo zao, Dk Mwakyembe aliwapongeza wazee hao kwa kuanzisha umoja huo na akawaahidi kuwasaidia kusambaza kwa wahisani andiko la mradi wa ujenzi wa kituo hicho ili azma yao hiyo itimie.

“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuandika upya historia ya watanzania kupitia program inayolenga kuyatambua maeneo ya urithi wa ukombozi ili yalindwe na kuhifadhiwa kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadae,” alisema na kuongeza kwamba hatua hiyo itasaidia historia ya Taifa isipotee.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment