Thursday, 5 April 2018

UVCCM MKOA WA IRINGA YAHAMASISHA VIJANA KUJIAJIRIUMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Iringa umewataka vijana wakiwemo wasomi wenye elimu ya juu kujiajiri kupitia kilimo na ufugaji kwa kuwa mahitaji ya bidhaa zitokanazo na sekta hizo ni makubwa kuelekea katika uchumi wa viwanda.

Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Kenani Kihongosi leo kwenye  kongamano la mafunzo na maonesho ya bidhaa za ujasiriamali kwa wananchi wa Iringa.

Kongamano hilo linalofanyika kwa siku tatu katika jumba la maendeleo mjini Iringa limeandaliwa na UVCCM Mkoa wa Iringa kwa udhamini wa kampuni ya kusindika maziwa ya Asas.

Kihongosi alisema haoni kama ni sahihi kwa kila msomi wa chuo kikuu kusubiri kuajiriwa ofisini wakati anaweza kutumia maarifa aliyonayo na ujuzi wa ziada kufanya shughuli za kujiajiri na kujipatia kipato kikubwa sambamba na kuajiri watu wengine.

“UVCCM bila kujali itikadi tumeamua kutoa mafunzo haya ya ujasirimali yatakayowaongezea ujuzi wananchi wa mkoa wa Iringa katika sekta hizo za kilimo na ufugaji lakini pia uzalishaji wa bidhaa za viwandani kama sabuni, jiki na batiki kwa kupitia viwanda vidogo vidogo,” alisema.

Kwa kupitia sekta ya kilimo, Kihongosi alisema mkoa wa Iringa una ardhi nzuri inayofaa kwa ufugaji na kilimo cha mazao ya chakula na biashara kama tumbaku, korosho, kahawa na chai.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela alisema katika kongamano hilo kwamba wajasiriamali wanaweza kuongeza tija katika shughuli zao kwa kuzingatia mambo makubwa matatu, kujengewa uwezo, kutengewa maeneo ya kufanyia shughuli zao na kupata mitaji.

Alisema kwa kupitia halmashauri zake serikali inao mpango wa kutenga asilimia 10 ya makusanyo yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na walemavu sambamba na kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za uwekezaji.

“Fursa hizo zipo na kila halmashauri inatakiwa kutenga maeneo ya biashara na uwekezaji, na vipo vikundi ambavyo tayari vimenufaika na mipango hii,” alisema katika kongamano hilo ambalo mgeni rasmi wake alitarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde.

Kasesela aligusia pia ahadi ya Sh Milioni 50 kwa kila kijiji iliyotolewa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na Rais Dk John Magufuli akiwataka wananchi kuwa wavumilibu.

“Mheshimiwa Rais hajamaliza miaka yake mitano ya kwanza, kuna mambo mengi anaendelea kuyafanya. Muwe na imani ahadi hiyo itatekelezwa kwasababu muda bado upo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment