Monday, 2 April 2018

T LED YAWEZESHA WAJASIRIAMALI WA IRINGA
WAJASIRIMALI 11 kati ya 182 waliofikiwa na Mradi wa Kuendeleza Wajasiriamali wa Ndani Tanzania (T LED) katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita mkoani Iringa watawezeshwa kutoka katika mradi huo asilimia 60 ya fedha za kununulia mashine bora za kuzalishajia bidhaa zao.

Wajasiriamali hao ambao kati yao asilimia 70 yake ni wanawake ni wale wanaojishughulisha na shughuli za uchakataji wa chakula, ufugaji wa kuku, ukamuaji mafuta ya alizeti na usindikaji wa sembe.

Taarifa hiyo ilitolewa na meneja mradi wa mikoa ya Iringa na Njombe, Stella Mdahila kwenye maonesho ya wajasiriamali wadogo na wa kati wa mkoa wa Iringa yaliyofanyika mjini Mafinga, wilayani Mufindi kwa uratibu wa mradi huo wa miaka mitano, ambao utekelezaji wake ulianza miaka mitatu iliyopita.

Maonesho hayo yaliyofanyika hivikaribuni katika viwanja vya mashujaa mjini humo yalifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza aliyelihimiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kuwalewa ipasavyo wajasiriamali wadogo ili kufanikisha azma ya serikali ya uchumi wa viwanda.

“Katika kuwawezesha wajasiriamali hao kupata teknolojia mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine zitaboresha uzalishaji wao, mchango wa T LED katika eneo hilo la kuchangia ununuzi wa mashine unakwenda hadi Sh Milioni 35,” alisema.

Mbali na mikoa ya Iringa na Njombe, alisema mradi wa T LED ambao umepata ufadhili kutoka serikali ya Canada unatekelezwa katika mikoa mingine nchini ukiwemo Mwanza, Shinyanga, Lindi na Mtwara.

Alitaja malengo ya mradi huo kuwa ni pamoja na kuhakikisha unawafikia wajasiriamali wadogo na wakati 1,760 katika mikoa hiyo na unatengeneza ajira 2,500 kupitia wajasiriamali watakaofikiwa na kuinua vipato vya wajasiriamali wapatao 1,300.

Katika kuharakisha kufikia malengo hayo, Mdahila alisema T LED inafanya kazi na wadau wakubwa watatu ambao ni SIDO, Chemba ya Wajasiriamali Wanawake Nchini (TWCC) na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).

Awali wajasiriamali hao ambao wengi wao ni wasindikaji wa vyakula walizungumzia changamoto zinazochelewesha biashara zao kupata vyeti vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Chakula na Dawa (TFDA) na masoko na kumuomba mkuu wa mkoa wa Iringa awasaidie kushughulikia changamoto hizo.

Mmoja wa wajasiriamali hao, Genovefa Barnabas wa kampuni ya FAMASHINE alitaja changamoto nyingine inayowakabili wafanyabiashara hao kuwa ni upatikanaji wa maeneo ya kuzalishia bidhaa zao na kufanyia maonesho ya bidhaa zao.

Katika kutatua changamoto hiyo, Mdahila alisema T LED kwa kushirikiana na SIDO imeanza ujenzi wa jengo la kisasa la uzalishaji mjini Iringa litakalowawezesha wajasiriamali wazawa wasio na maeneo, kupata eneo la kisasa la kufanyia uzalishaji.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment