Monday, 30 April 2018

SERIKALI YA DK MAGUFULI KUPAISHA UTALII WA KUSINI


RAIS  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DkJohn Magufuli ametaja moja ya vipaumbele vya serikali yake kuwa ni pamoja na kupanua wigo wa vivutio vya utalii kusini mwa Tanzania ili sekta hiyo ichangie zaidi kwenye pato la Taifa na kuondoa umasikini katika jamii.

Aliyasema hayo mara baada ya kuizindua Barabara  ya Iringa Migori Fufu ambayo ni sehemu ya barabara ya Iringa Dodoma yenye urefu wa Kilometa 260, katika ziara yake iliyoanza jana mkoani Iringa, itakayokwenda sambamba na kushiriki maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kitaifa yatafanyika mjini Iringa kesho.

Alisema kwa kupitia mkakati huo alisema serikali yake imedhamiria kuufungua utalii wa ukanda wa kusini ambao kitovu chake ni mkoani Iringa kwa kuboresha vivutio na miundombinu.

 “Tumeamua kuukarabati uwanja wa ndege wa Nduli ili uwe wa mkubwa na wa kisasa tutajenga barabara ya lami ya Iringa hadi katika geti la hifadhi ya Taifa ya Ruaha hatua itakayowezesha wageni wengi kuitembelea,” alisema.

Ukarabati wa uwanja wa ndege wa Nduli na barabara ya Iringa hadi katika geti la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni hifadhi kubwa kuliko zote nchini utafanywa kupitia mradi wa REGROW uliozunduliwa Februari mwaka mjini Iringa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa kupitia mradi huo, Benki ya Dunia imetoa mkopo nafuu wa dola za kimarekani Milioni 150 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh Bilioni 340 za Kitanzania kwa ajili ya kusimamia maliasili na kuendeleza utalii wa ukanda wa Kusini.

Mbali na kutengeneza ajira, Dk Magufuli alisema itakapokamilika, mipango hiyo itachochea shughuli za utalii na kuvutia idadi kubwa ya watalii.

Alitoa wito kwa watanzania hususani wa mkoa wa Iringa na mikoa jirani kuanza kujiweka sawa ikiwa ni pomoja na kupata mafunzo ya utalii ili waweze kunufaika na fursa hiyo.

“Ni wajibu wetu kuwahimiza na kuwashawishi vijana wetu wajihusishe na masuala ya utalii ikiwa ni pamoja na kujifunza lugha mbalimbali za nje kama Kispaniola, kifaransa, kijerumani na kingereza,” alisema.

Akitoa mfano wa jinsi vijana wa Zanzibar wanavyonufaika na shughuli za utalii, Dk Magufuli alisema wengi wao wanafanya kazi ya kuongoza watalii baada ya kuiona fursa hiyo na kuichangamkia.

Kwa mujibu wa taarifa za Serikali, sekta ya utalii ina mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa ambapo huchangia zaidi ya asilimia 17 kwenye pato la Taifa, asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni na asilimia 12 ya ajira zote nchini.


Mbali na kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, Dk Magufuli atatumia ziara yake ya siku tano mkoani Iringa kuweka jiwe la msingi ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kilolo, kuzindua kiwanda cha uzalishaji wa chakula cha kuku cha Silverland na kufungua barabara ya Iringa Mafinga.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment