Tuesday, 3 April 2018

RDO YAWEZESHA KIJIJI CHA NANDALA MUFINDI KUPATA MAJI SAFI


MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amezindua mradi wa maji utakaowanufaisha watu zaidi ya 1,000 katika kijiji cha Nandala kilichopo zaidi ya Kilometa 50 kutoka makao makuu ya wilaya ya Mufindi, mjini Mafinga mkoani Iringa.

Mradi huo umejengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 95.5 kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo Vijijini (RDO) linalopendekeza kuwepo kwa mamlaka za maji vijijini ili kusogeza huduma kwa watu.

Pamoja na pendekezo hilo, Mratibu wa RDO, Fidelis Filipatali aliishauri serikali kuondoa kodi kwenye manunuzi ya malighafi za maji zinazotumika kwa ajili ya miradi ya maji na kupunguza urasimu wa vitengo vingi kwenye idara ya maji unaochelewesha upatikanaji wa vibali.

Akiwaomba wananchi wa kijiji hicho kuthamini maji ya bomba, aliwataka wapunguze matumizi ya maji ya visima, mito, mvua na chemichemi na serikali itilie mkazo uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu zinazofanywa.

Alisema licha ya mradi wa RDO kupeleka mradi wa maji katika kijiji cha Nandala, mradi huo umewezesha upatikanaji wa huduma hiyo katika kijiji cha Ikonongo, Ludilo, Kidete, Ikanga, Ubwanzi, Isipii na Mkonge kwa wilaya ya Mufindi na Lulanzi,  Kuhindo, Barabara mbili na Isele kwa wilaya ya Kilolo,” alisema.

Alisema ili miradi hiyo ya maji iwe endelevu ni muhimu kwa watumiaji maji kuchangia na kutilia mkazo elimu ya maji wanayopata kutoka kwa wataalamu.

Akizindua mradi huo Mkuu wa Mkoa alipiga marufuku shughuli za kibinadamu zinazofanyika kwenye vyanzo vya maji akisema uamuzi huo utaongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo kwa muda mrefu.

“Nataka sheria ya maji itumike, na mtumishi yoyote wa umma anayepata kigugumizi cha kutumia sheria hiyo katika kuhifadhi vyanzo vya maji, aondoke. Hii sio hiari, na wala sibembelezi, nataka kuona vyanzo vya maji vinahifadhiwa,” alisema.

Akitoa takwimu za upatikanaji maji mkoani Iringa, Mhandisi wa Maji wa Mkoa wa Iringa, Shaban Jellan alisema watu 670,348 mijini na vijijini sawa na asilimia 71 ya wakazi wote wa mkoa wa Iringa wanapata maji ndani ya umbali usiozidi mita 400.

Alisema uendelevu wa miradi ya maji unategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa vyombo imara vya kisheria vya watumiaji wa maji.

“Hadi sasa mkoa una kamati za maji 185, mifuko ya maji 156 na jumuiya za watumia maji 44 zenye jumla ya zaidi ya Sh milioni 65,” alisema na kuongeza kwamba kwa kupitia halmashauri wanaendelea na juhudi za kusajili jumuiya za watumiaji maji.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment