Sunday, 8 April 2018

MAZIWA YA ASAS YAONGEZA FURSA KWA VIJANA WA IRINGA
KAMPUNI ya Maziwa ya Asas imetumia kongamano la mafunzo na maonesho ya bidhaa za ujasiriamali wa mjini Iringa kuhamasisha unywaji maziwa  na kufungua milango kwa wajasiriamali wanaotaka kujishughulisha na uuzaji wa bidhaa za maziwa zinazozalishwa na kampuni hiyo.

Kongamano hilo la siku tatu lililokusanya wajasiriamali zaidi ya 1,000 waliokuwa wakipewa maziwa ya kampuni hiyo kila siku lilifanyika katika ukumbi wa Jumba la Maendeleo, mjini Iringa kwa uratibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Iringa.

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Ahmed Salim Abri alisema wakati kongamano hilo likifungwa jana kwamba maziwa yanayosindikwa na kiwanda chao yamechochea ufugaji na yamekuza ajira ya ndani na nje ya kiwanda hicho kilichopo mjini Iringa.

“Vikundi vya wajasiriamali vinavyotaka kufanya biashara ya maziwa yaliyosindikwa na kampuni yetu niwaambie fursa hiyo ipo,” alisema na kutoa mfano wa mjasiriamali Hashim Habibu aliyebadili maisha yake baada ya kuanza kuuza maziwa ya kampuni hiyo.

Akitoa ushuhuda katika kongamano hilo, Habibu alizungumzia maisha yake yalivyokuwa ya taabu kabla hajapata fursa ya kujiingiza katika biashara hiyo na namna yalivyobadilika baada ya kuanza biashara hiyo.

“Siwezi kuacha kufanya biashara hii; kwa miaka mitano tu najivunia uvumilivu na malengo niliyojiwekea yameniwezesha kujenga nyumba ya vyumba vitatu na nimenunua bodaboda inayonisaidia kusambaza bidhaa hizo kwa wateja wangu,” alisema.

Akifunga kongamano hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Antony Mavunde aliipongeza kampuni ya Asas kwa kuchochea ajira kwa vijana na akazikumbusha halmashauri zote nchini kuendelea kutenga asilimia 10 ya fedha za mapato yao ya ndani kila mwaka kwa ajili ya kuwakopesha akina mama, vijana na walemavu.

“Pia nawaomba wakurugenzi wa halmashauri mtenge maeneo maalumu yatakayoyawezesha makundi hayo kufanya na kuendeleza shughuli zao za ujasirimali zikiwemo zile zinazozalishwa na makampuni mengine na wanazozalisha wenyewe,” alisema.

Awali Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa Kenani Kihongosi alisema kwa kupitia kongamano hilo ambalo yeye alikuwa mmoja wawezeshaji wake, wajasirimali hao wamefundishwa kilimo na ufugaji wenye tija na utengenezaji wa bidhaa za viwandani kama sabuni, jiki , batiki na vyakula zikiwemo keki.

Katika risala ya UVCCM Mkoa wa Iringa iliyosomwa kwa waziri huyo na Katibu wa Seneti ya Vyuo Vikuu vya Iringa,
Shaibath Kapingu , vijana hao waliomba msaada wa Sh Milioni sita kwa ajili ya kufanikisha ukarabati jengo lao kitega uchumi lililopo katikati ya mji wa Iringa.

Akiitikia ombi hilo, Mavunde aliahidi kuchangia Sh Milioni nne na akaagiza Sh Milioni mbili zilizobaki zitafutwe na mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela aliyeahidi kutafuta fedha hizo kwa kushirikia na CCM Manispaa ya Iringa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment