Friday, 20 April 2018

MAANDALIZI YA MEI MOSI YASHIKA KASI, DK MAGUFULI MGENI RASMIMKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewaomba wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais Dk John Magufuli anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Sherehe za Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yatakayofanyika katika uwanja wa Samora, mjini Iringa.

Pamoja na kushiriki maadhimisho hayo, hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kukanyaga ardhi ya mkoa wa Iringa tangu achaguliwe kushika wadhifa huo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Akizungumza na wanahabari mapema leo, Masenza amesema; “Mkoa wa Iringa umechaguliwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kitaifa. Hii ni heshima kubwa kwa mkoa wetu kupata fursa hii adhimu.”

Alisema maadhimisho hayo yatatanguliwa na michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba na kutakuwepo na bonanza la michezo mbalimbali.

“Michezo hiyo inayoshirikisha watumishi wa sekta mbalimbali za umma na binafsi ilianza April 17 na itahitimishwa April 30, siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho hayo,” alisema.

Aidha alisema, sherehe hizo za Mei Mopsi zitahusisha maonesho ya shughuli mbalimbali za wafanyakazi, taasisi za umma na binafsi, wawekezaji na wajasiriamali katika uwanja wa Kichangani, Kihesa mjini Iringa.

Akielezea  maandalizi ya  sherehe hizo, alisema kamati mbalimbali zimeundwa kwa maandalizi ya shughuli zote zitakazofanyika kabla na wakati wa maadhimisho.

“Maandalizi yanakwenda  vizuri na  wamepata  ratiba ya  kuzunguka  wilaya  zote za  mkoa  wa Iringa kutoa elimu  pamoja na kututana na  wafanyakazi ili  kujua  changamoto  zao,” alisema.

“Tumejiridhisha kuwa kila kitu kinaenda kama tulivyopanga ndio maana leo tuna uhuru wa kusema kuwa Mei Mosi hii itafanyika kwa mafanikio makubwa mno,” alisema

Aliwataka  wafanyakazi   kujitokeza  kwa  wingi  kushiriki sherehe  hizo  zitakazowawezesha pia kujua mikakati mbalimbali inayolengwa na  serikali katika kuboresha hali za wafanyakazi nchini.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni  “Kuunganishwa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Nchini Kulenge Kuboresha Mafao ya Wafanyakazi,”


Reactions:

0 comments:

Post a Comment