Wednesday, 18 April 2018

KIWANDA CHA IVORI CHAPAISHA ULAJI WA CHOCOLATE NCHINI

WAKULIMA wa zao la Cocoa (Kakao), wanasema ni miongoni mwa watanzania walio wengi ambao hivisasa wanaijua ladha ya Chokoleti (Chocolate) zinazozalishwa kutokana na zao hilo linalolimwa kwa wingi katika wilaya za Rungwe na Kyela mkoani Mbeya.

Mmoja wa wakulima wa zao hilo wa kijiji cha Ipinda, wilayani Kyela, Godwin Mwakajileke (67) anasema; “Zamani tulihamasishwa kulima zao hili la kibiashara tukielezwa ni kwa ajili ya matumizi ya soko la nje.”

Mwakajileke anasema wapo wakulima waliokuwa wanajua matumizi ya Cocoa katika soko la nje, lakini yeye binafsi hakuwahi kujua kama zao hilo ndilo linalotumika kutengeneza Chokoleti.

 “Nilijua matumizi hayo miaka ya karibuni baada ya kampuni ya Iringa Food and Bevarage ya mjini Iringa ilipoanza kununua zao hilo wanalotumia kutengenezea Chokoleti aina ya Ivori ambayo pia inapatikana katika maduka ya hapa kijijini,” anasema.

Mkurugenzi wa kampuni ya IVORI Ltd, Suhail Esmail Thakore anasema zao la kakao ambalo hutokana na mti wa Theobroma ndilo linalotumika kutengenezea chokoleti ambayo hutafsiriwa kama ‘chakula cha miungu’.

Thakore anasema punje za Cocoa hutumika kutengeneza Cocoa bata (Cocoa butter) na Unga wa Cocoa (Cocoa Powder).

Pamoja na Cocoa bata kutumika kutengeneza Chokoleti katika maeneo mengine hutumika kutengeneza vipodozi zikiwemo sabuni na krimu.

Na kwa upande wa unga wa Cocoa, anasema hutumika kama kiungo cha kuongeza ladha kwenye vyakula na vinywaji kama ice cream, biskuti, keki na pipi.

“Lakini pia maganda yake hutumika kama chakula cha wanyama, mbolea na kutengeneza viwanyaji vya aina mbalimbali,” anasema.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kakao (ICCO) nchi za Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Cameroon ndio wazalishaji wakubwa wa Cocoa barani Afrika na hapa nchini asilimia 95 ya zao hilo hulimwa mkoani Mbeya.

Taarifa ya ICCO ya mwaka 2014/2015 inakadiria Tanzania huzalisha zaidi ya tani 7,000 kila mwaka ambazo ni sehemu ndogo ya uzalishaji wote unaofanyika katika nchi za Afrika Magharibi ambao ni zaidi ya tani milioni 2.5 kwa mwaka.

Taarifa hiyo inasema asilimia 90 ya chokoleti yote inayotengenezwa duniani hutumiwa na nchi zilizoendelea zikiwemo za Ulaya, Asia na Amerika pamoja na kwamba asilimia 70 ya chokoleti hiyo hutokana na Cocoa inayozalishwa barani Afrika.

Hapa nchini, Thakore anasema Chokoleti ambayo matumizi yake yalikuwa yakidhaniwa ni kwa ajili ya watu wenye uwezo zaidi ilikuwa ikiagizwa kutoka nje ya nchi na ilikuwa ikipatikana kwa bei ya juu kwenye maduka makubwa ya vyakula (Super Markets).

“Mambo yanazidi kubadilika, hivi sasa Chokoleti aina ya Ivori inapatikana kwa bei nafuu kabisa mijini na vijijini, hiyo ikiwa ni baada ya kampuni yetu kujenga mjini Iringa kiwanda kinachozalisha bidhaa hiyo,” anasema.

“Hiki ni kiwanda cha kwanza kujengwa Tanzania na Afrika Mashariki. Tunaendelea kupambana ili kisaidie kukuza soko na matumizi ya Chokoleti tunazozalisha; ndani na nje,” anasema.

Februari mwaka huu, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alitembelea kiwanda hicho na akapongeza uwekezaji wake akisema ni cha mfano wa mapinduzi ya viwanda yanayoendelea nchini.

“Nipongeze kiwanda hiki, kitakuwa nguzo ya uchumi kwa wazalishaji wa Cocoa nchini, kitasaidia kuongeza ajira kiwandani na mashambani kwa kadri uzalishaji wake utakavyokuwa ukiongezeka,” anasema.

Naye Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya aliyetembelea kiwanda hicho hivikaribuni anasema; “Kutokana na ongezeko la mahitaji ya chokoleti nchini wajasiriamali wa Tanzania wanaweza kutumia fursa ya kuzalisha Cocoa kwa wingi ili kutengeneza kipato cha familia.”

Manyanya anasema fursa hiyo lazima iendane na kuhimiza matumizi ya chokoleti nchini ikizingatiwa kwamba mbali na wilaya za Kyela na Rungwe, Tanzania ina maeneo mengine mengi ikiwemo Morogoro na Kigoma yanayofaa kwa kilimo hicho.

“Fursa ya uzalishaji na usindikaji wa Cocoa ikitumiwa vizuri itaiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia. Lakini pia itachochea utekelezaji wa sera ya viwanda inayokusudia kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025,” anasema.

Masoko na mipango ya baadaye
Thakore anasema Kiwanda hicho kinachotumia sehemu ya asilimia tano ya Cocoa yote inayozalishwa kila mwaka hapa nchini kinazalisha asilimia 30 tu ya mahitaji ya soko.

Mbali na Chokoleti, Thakore anasema kiwanda hicho kinazalisha Unga wa Cocoa, pipi na bidhaa zingine za kuongeza ladha katika vyakula zikiwemo tomato sause na chill sause, zote zikifahamika kwa jina la Ivori.

Anasema katika kipindi cha miaka michache iliyopita, kumekuwepo na ongezeko la matumizi ya bidhaa hizo ndani ya nchi, na nje ya nchi mahitaji yake ni makubwa katika nchi jirani za Kongo, Rwanda, Kenya, Burundi na Uganda.

“Bidhaa zetu zinashindana vizuri na bidhaa za nje, huo ni mwelekeo tosha kwamba ubora wake unaweza kuzidi ubora wa zile zitokazo nje,” anasema.

Akitoa mfano wa mahitaji ya soko la nje, mwekezaji huyo mzawa anasema walitakiwa na wafanyabiashara wa Burundi kusambaza tani 30 za bidhaa hizo kila mwezi lakini wanashidwa kwasababu uzalishaji wa sasa hauwawezeshi kufikia kiwango hicho.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo na kuunga mkono azma ya Rais ya Tanzania ya Viwanda, anasema wako katika hatua ya mwisho ya kukamilisha ujenzi wa kiwanda kipya cha pipi kitakachowawezesha kufikia hadi asilimia 50 ya mahitaji ya soko huku upanuzi wa viwanda vya bidhaa zao zingine zikiwemo Chokoleti, ukiwa katika mipango yao ya mwaka 2019/2020.

“Katika kuongeza uzalishaji tumeanza kupanua viwanda vyetu, upanuzi utakaokwenda sambamba na ongezeko la malighafi ikiwemo sukari ya matumizi ya viwanda ambayo kwasasa haizalishwi nchini,” anasema.

Akizungumzia ubora na azma ya kupata masoko hadi nje ya bara la Afrika, Thakore anawataka watanzania wawe wazalendo kwa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini akisema faida zake ni nyingi ikiwemo kukuza uchumi wa nchi na wa watu wake.

Ajira
Thakore anasema kwasasa kiwanda chao pamoja na kiwanda mama cha Ivori Ltd kwa pamoja vimeajiri wafanyakazi 150.

“Idadi ya wafanyakazi hao itaongezeka hadi zaidi ya 300 tutakapokamilisha upanuzi wa viwanda vyetu mwaka 2020,” anasema.

Kwa upande wa pili wa wakulima, Thakore anawataka wakulima kutumia fursa ya kiwanda chake kuboresha uzalishaji wa Cocoa ili wajihakikishie soko la ndani na nje pia.

Anasema Tanzania ikijidhatiti na kuwekeza kwenye Cocoa uwezekano wa kubadilisha maisha ya wakulima kiuchumi ni mkubwa kwa kuwa zao hilo lina soko kubwa ndani na nje ya nchi japokuwa uzalishaji wake ni mdogo.

Mmoja wa wakulima wa zao hilo kutoka kijiji cha Ipanda wilayani Kyela, Steven Kaoneka anasema anafikiria kuongeza ukubwa wa shamba lake kutoka heka mbili za sasa hadi tano baada ya kuhakikishiwa soko na kampuni hiyo.

Mchango katika jamii
Mbali na kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutoka na shughuli za kampuni hiyo, Thekore anasema; “tunashiriki kikamilifu katika shughuli zingine za maendeleo ndani ya jamii inayotuzunguka.”

Akifafanua anasema kampuni imekuwa ikichangia maendeleo ya sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, afya, miundombinu na usalama.

Mmoja wa majirani wanaoishi jirani na kiwanda hicho kilichopo eneo la viwanda la Ipogolo mjini Iringa, John Luoga anasema;  “Uwepo wa kiwanda hiki katika eneo hilo umetusaidia wananchi wa jirani kwani kinasaidia shughuli mbalimbali za maendeleo kwa mfano kilijenga kituo cha Polisi ili kusaidia kushughulikia matukio ya uhalifu.”

Je analipa kodi?
Kuhusu kodi, Thakore anasema kiwanda chao ni moja ya walipaji wakubwa wa kodi mkoani Iringa na wanatimiza wajibu huo kwa kuwa wanajua mchango wa kodi katika ujenzi wa huduma za jamii.

“Niwahimize wafanyabishara wenzangu na wananchi kwa ujumla tulipe kodi. Misaada tunayopata kutoka nchi zilizoendelea ni kodi za wananchi wa kule, tuwe na utamaduni huo na hayo ndio maendeleo,” anasema.

Anasema hakuna serikali yoyote duniani inayoweza kutoa huduma muhimu kwa watu wake kama watu wake watakuwa hawalipi kodi.

Azma ya serikali ya awamu ya tano

Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili kuongeza kasi ya kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 inayolenga kuifanya nchi kuwa yenye hadhi ya kipato cha kati na kuondokana na umaskini.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza anasema “ili kufikia Dira hiyo wazalishaji wanatakiwa kuongeza tija katika uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kuvutia masoko ya ndani na nje ya nchi na wanatakiwa kulipa kodi ipasavyo.”

Masenza anasema siri ya mafanikio hayo ambayo kampuni ya Iringa Food and Bevarage Ltd na Ivori Ltd imeanza kuyapata ni kuhakikisha wawekezaji wanakuwa na mifumo ya uzalishaji wenye tija inayofuatwa ili kuleta  matokeo ya uzalishaji wenye viwango vya kimataifa.

Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Iringa, Lucas Mwakabungu ameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kukaa na wafanyabiashara, kusikiliza kero zao na kuzitafutia changamoto.

“Hatua iliyofanywa hivikaribuni na Rais Dk John Magufuli ya kukutana na wawekezaji mbalimbali imefungua milango itakayoongeza kasi katika kushughulikia kero mbalimbali za uwekezaji,” anasema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment