Tuesday, 3 April 2018

MCHUNGAJI MSIGWA, MEYA WASUBIRIWA MAHAKAMANI IRINGA

Image result for Mchungaji msigwa na mstahiki meya


KESI mbili za jinai zinazomkabili Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) zimehairishwa leo hadi Mei 3 huku ile inayomkabili Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe (Chadema) nayo ikiahirishwa hadi April 10 kwa kuwa hakimu, John Mpitanjia anayeisikiliza hayupo.

Wakati mstahiki meya anatakiwa kuanza kujitetea katika kesi hiyo Namba 189 ya mwaka 2017, kesi za Mchungaji Msigwa aliyeshitakiwa pamoja na wafuasi wengine wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zimeahirishwa kwa kile kilichoelezwa uchunguzi wake bado haujakamilika.

Kesi ya mstahiki meya ya kutishia kumuua kwa bastola aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Manispaa ya Iringa, Alphonce Muyinga inasikilizwa katika mahaka ya wilaya Iringa.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, David Ngunyale, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Magreth Mahundi aliiambia mahakama hiyo kwamba katika kesi Namba 6 ya mwaka 2018, Mchungaji Msigwa anashitakiwa pamoja na wenzake sita kula njama za kutenda kosa na kuharibu mali.

Katika tukio hilo, Mahundi alisema Mchungaji Msigwa pamoja na Patrick Madati, Samwel Nyunda, Leonce Marto, Rody Mtakima, Sophia Lupembe na Rehema John walikula njama kati ya Januari 4 na 15 na Januari 15 wakatenda kosa la kubomoa nyumba ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mwangata, Anjelus Mbogo iliyopo Igumbilo mjini Iringa.

Mbogo alijivua udiwani na uanachama wa Chadema na kutimkia Chama cha Mapinduzi (CCM) siku chache kabla ya kutokea kwa tukio hilo.

Katika kesi namba 7 ya mwaka 2018, mwendesha mashtaka alisema Mchungaji Msigwa pamoja na Dama Msigwa, Agrey Mkemwa, Maneno Rashid, Deogratius Kibumu, Tikatika Kilage na Lwimso Kadenga walikula njama kati ya Januari 4 na 15 na Januari 17 walitenda kosa la kuchoma moto nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha.

Nyumba hiyo iliyopo Kihesa Mjini Iringa alikuwa akiishi aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Manispaa ya Iringa, Alphonce Muyinga pamoja na wapangaji wengine wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo).

Akiomba kuahirishwa kwa kesi hizo, Mahundi aliiomba mahakama hiyo iongeze siku za kufanyia uchunguzi mashauri hayo baada ya siku 60 za kisheria kwisha huku uchunguzi wake ukiwa haujakamilika.

“Mheshimiwa Hakimu tunaomba muda zaidi wa uchunguzi wa kesi hizi kwasababu upande wa upelelezi bado unaendelea na uchunguzi wa matukio hayo katika mitandao,” alisema.

Akiahirisha kesi hizo hadi Mei 3, Hakimu Ngunyale alishangazwa kuchelewa kwa uchunguzi wa kesi hizo ambazo matukio yake yametokea maili zisizozidi tano toka katikati ya mji wa Iringa.

Ngunyale aliutahadharisha upande wa mashtaka akisema mahakama sio sehemu ya kuegesha kesi ni sehemu ya kusikiliza kesi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment