Thursday, 5 April 2018

JUKWAA LA WAHARIRI LAHUZUNIKA UHURU WA HABARI KUMINYWA

Image result for Deodatus Balile


JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limesema matukio yanayoendelea nchini yakiwamo ya kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari, utekaji, mauaji na kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa hayana afya kwa Taifa.

TEF imesema ili kujikita kwenye agenda ya Taifa ya Tanzania ya viwanda, ipo haja kwa Serikali kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii kujadiliana kuhusu mustakabali wa amani na maridhiano ya kitaifa.

Akitoa taarifa kuhusu hali ya uandishi wa habari nchini leo Alhamisi Aprili 5, 2018 Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema jukwaa hilo lilijadili na kutafakari kwa kina hali halisi ilivyo nchini ambayo inaibua sintofahamu na malalamiko kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii.

Amesema malalamiko hayo ambayo baadhi yake yameripotiwa kwenye vyombo vya habari, yanagusa sehemu kuu tatu ikiwamo kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni hasa kupitia vyombo vya habari, kuzorota kwa demokrasia na ukuaji wa uchumi usioakisi hali halisi ya maisha ya watu.

 "Tunayo mifano ya nchi nyingi duniani zikiwamo zile ambazo ni majirani zetu ziliingia katika gharama kubwa kwa kudharau matukio madogo madogo kama ambayo yanatokea nchini hivi sasa," amesema.

Balile katika taarifa hiyo amesema ni vizuri kujifunza kwa nchi nyingine kwamba vyombo vya dola vinaweza kufanya kazi vizuri vikiwa vinaungwa mkono na raia wa Taifa husika.

“Kama ambavyo Rais John Magufuli alivyokutana na wafanyabiashara hivi karibuni, kuna haja ya kukutana na makundi mengine muhimu kwenye jamii yetu," amesema.

Ametaja makundi mengine kuwa ni wanaharakati, viongozi wastaafu, wakuu wa vyama vya siasa, taasisi za dini, asasi za kiraia, vyama vya kitaaluma yakiwamo makundi rika ya wazee na wanawake, vyombo vya dola na makundi mengine muhimu

Reactions:

0 comments:

Post a Comment