Sunday, 8 April 2018

JICHO LA MICHAEL MLOWE KATIKA SEKTA YA MICHEZO TANZANIA

Image result for Michael Mlowe


Nawaza kama nchi tunakosea wapi, nini kinatuzuia kufika mbali kimichezo? 

Ni kitu gani wanacho wenzetu wa Angola, nchi ambayo imepigana vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka 21 lakini wameweza kushiriki kombe la Dunia na lile la Mataifa Huru ya Afrika.

Ni kitu gani tunajifunza kwa nchi za jirani mfano Kenya, Uganda na hata Ethiopia.. kwanini wapo vizuri katika michezo mingi ikiwemo riadha?

Nawaza tena na tena, viongozi wa Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni, waliopita na waliopo, wanaichukuliaje hali hii?

Narudi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wapo wapi, na wanawaza nini kutuondoa hapa tulipo na kutupeleka kwenye mafanikio?

Naiangalia jamii (Watanzania Milioni 55) tunawaza nini, ni kwa muda gani tutaendelea kuwa na timu wasindikizaji katika michuano mingi ya kimataifa?

Narudi kwa wadau wengine na taasisi zingine zenye mchango katika sekta hii, nao wanawaza nini juu ya hali hii?

Kama Taifa ni lazima tujiulize wapi tunakosea, najiuliza ni lini Tanzania tutabadilika na kuwa washindani na si wasindikizaji ili tusiendelee kutia aibu katika sekta hii ya michezo??

Mimi naanza kwa kulia na hawa makocha wa kigeni, wanalipwa fedha nyingi ila wengi wao uwezo wao huwezi kuutofautisha na walimu wengi wa hapa nchini.

Vuta mfano timu kubwa kama Yanga  na Simba ambazo kwa hapa nchini zimekuwa kinara wa kuajiri makocha wakigeni, mbona mara kadhaa zimekuwa zikifungwa na makocha wazalendo wa timu zingine zikiwemo zisizo na majina kabisa nje ya mipaka ya nchi?

Nawaza tu huenda tukiweka mfumo wa kuwalipa vizuri makocha wetu lipo jambo litatokea mbele ya safari.

Pili niiombe wizara ya michezo pamoja na baraza la michezo kuangalia upya sera za michezo Tanzania...

Michezo ni ajira na michezo ni afya, vijana wetu hawafiki mbali katika sekta hiyo kwasababu hatuna misingi iliyo bora toka chini kabisa. 

Ni aibu kwa shule za msingi kukosa mipira na vifaa vya michezo katika zama hizi za mapinduzi ya michezo na matumizi ya teknolojia kubwa. 

Tukumbuke michezo ni ajira, Tanzania ikifanikiwa kimichezo tutakuwa tumepanua wigo wa ajira kupitia sekta hii ya michezo na hivyo kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kutengeneza ajira mpya kwa kadri inavyowezekana.

Tukiongeza wigo na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa sekta ya michezo, tutafungua ajira kwa vijana, serikali itapata kodi zake na kutakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya uchumi wan chi.

Nampongeza Mbwana Samatta kwa kufika pale, tungependa vijana wengi wapate mafanikio aliyonayo na kuliletea Taifa sifa kubwa.

Na tatu ni muhimu tukakumbuka michezo ina maadili yake, kwa kuzingatia maadili hayo tutavuna tulichopanda. Kwahiyo tusiendelee kuyasahau maadili hayo na tusisubiri miujiza kupata mafanikio.

Michezo (pyramid of sports) inajengwa kwa kuzingatia mambo yafuatayo 

FOUNDATION 
Hapa vijana hujazana kwa wingi kwa kuwa ni eneo la kwanza la kujua aina ya michezo  ambayo vijana wanaweza kushiriki

PARTICIPATION 
Katika eneo hilo, wengi hushiriki michezo mbalimbali na ndio chimbuko la kujua au kupata vipaji

PROFFESIONALISM 
Katika eneo hilo, namba hupungua kwani ni eneo la mashindano ya ngazi mbalimbali na hapa ndipo vipaji huanza kuonekana na kutumiwa

EXCELLENCE 
Eneo hili huwa na watu wachache sana, hawa ni wale wenye juhudi, nidhamu na wanaozingatia maadili ya kile wanachofanya

Tanzania tunaweza kuutumia mzunguko huo, kugundua vipaji na kuviendeleza na kufikia kilele cha mafanikio tunayoyataka. 

Nashauri wadau na serikali kwa ujumla tushiriki kuziangalia upya sera zetu za michezo na kuyafanyia kazi mapungufu yake ili zifanye kazi itakayokuwa na matokeo chanya mbele ya safari.

Hii itasaidia vijana wasilalamike, wadau wasilalamike na vyombo mbalimbali vinavyosimamia michezo ikiwemo TFF nao wasilalamike.

Michael Mlowe ni Mdau wa michezo na Mwakilishi wa vilabu(mpira wa miguu) manispaa ya Iringa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment