Wednesday, 21 March 2018

SERIKALI YATAFUTA KITANDA ALICHOLALIA NELSON MANDELA KILOLOSERIKALI imeahidi kutafuta kilipo kitanda alicholalia rais wa kwanza mwafrika wa Afrika Kusini Nelson Mandela katika kituo cha wapigania uhuru wa taifa lake katika kijiji cha Kihesa Mgagao wilayani Kilolo, mkoani Iringa ili kiwe sehemu ya kumbukumbu ya maeneo ya urithi wa ukombozi wa bara la Afrika. 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe aliyasema hayo katika ziara yake aliyofanya wilayani Iringa na Kilolo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akitembelea maeneo hayo ya ukombozi.

Mandela aliyefariki Desemba 5, 2013 akiwa na miaka 95 alitembelea na kulala katika kituo hicho kinachotumiwa kama gereza la wilaya ya Kilolo, Machi 1990 akiwa na aliyekuwa mkewe Winnie Mandela wakati wa ziara yake nchini baada ya kuachiwa huru na utawala wa makaburu.

Pamoja na Mandela na mkewe Winnie, Dk Mwakyembe alisema rais wa sasa wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na wapigania uhuru wengine maarufu, waliishi kwa muda katika kituo hicho.

“Kituo hiki kinatengeneza historia kubwa ya kukumbuku ya maeneo hayo, naunga mkono kisiendelee kuwa gereza na niahidi pia tutakitafuta kitanda hicho na kukirejesha hapo,” alisema huku akiomba halmashauri ya wilaya ya Kilolo kutafuta eneo mbadala patakapojengwa gereza jingine ili kufanikisha mpango huo.

Alisema kwa kupitia mpango huo, chumba alicholala Mandela na rais wa sasa wa Afrika Kusini navyo vitatengezwa vizuri ili viwe sehemu ya utalii na viliingizie Taifa mapato stahiki kutoka kwa wageni watakaotembelea.

Pamoja na kukitambua kituo hicho cha Kihesa Mgagao, Dk Mwakyembe alisema wizara yake imekwishayatambua maeneo ya urithi wa ukombozi 161 yatakayohifadhiwa kwa nguvu zote ili kulinda historia yake. 

Mbali na mpango huo wa kitaifa alisema serikali iko katika mchakato wa ujenzi wa kituo kikuu cha urithi wa ukombozi wa bara la Afrika unaolenga kutekeleza azimio lililotolewa na Umoja wa Afrika mwaka 2011 kwa kuzingatia mchango wa Tanzania katika ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika.

Alisema kituo hicho kitakachokuwa na maktaba kubwa itakayokuwa na historia yote na vituo vikubwa vya Tehama , utafiti na kumbukumbu za nyaraka kimepangwa kujengwa katika eneo la Magwepande au Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Wakati mchakato huo ukiendelea, alisema wasimamizi wa program wamekwisha kusanya picha zaidi ya 3,000 za historia ya ukombozi na wamehoji wazee 201 akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa; walioona na kushiriki vita au harakati mbalimbali za mapambano.

Awali katika risala yao iliyosomwa kwa waziri huyo na Afisa Mtendaji wa kijiji cha Kihesa Mgagao, Anna Mwinuka, wananchi wa kijiji hicho walisema kuweka gereza mahali ambapo watu wengine walipatumia kuendesha harakati za kudai uhuru, hakuenzi juhudi hizo na badala yake kunapoteza historia yake.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah alisema pamoja na kuondoa gereza hilo, wananchi wanaomba katika kituo hicho pajengwe pia taasisi zinazoweza kusaidia maendeleo ya kijiji ikiwemo shule na chuo cha ufundi, na yatengwe maneo maalumu kwa ajili ya akina mama, vijana walemavu na wajasriamali yatakayotumiwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo


Reactions:

0 comments:

Post a Comment