Wednesday, 21 March 2018

SERIKALI YAPOKEA MALALAMIKO YA FAMILIA YA CHIFU MKWAWA


SERIKALI imeahidi kushughulikia malalamiko ya familia ya chifu wa wahehe, Mtwa Mkwawa yaliyoelezwa  kuchangia kuzorotesha uendelezaji na uendeshaji wa makumbusho ya chifu huyo yaliyopo katika kijiji cha Kalenga, wilayani Iringa mkoani Iringa.
 

Taarifa ya malalamiko hayo ambayo hata hivyo hayakuelezwa kwa kina na familia hiyo, yalikabidhiwa kwa maandishi hivikaribuni kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na mmoja wa vitukuu wa Chifu Mkwawa, Fatuma Mkwawa .

Fatuma Mkwawa ni mmoja kati ya watoto marehemu Chifu Abdul Adam Sapi Mkwawa aliyefariki Februari 14, 2015.


Dk Mwakyembe alitembelea makumbusho hiyo ambako pamehifadhiwa fuvu la chifu huyo katika ziara yake aliyofanya wilayani Iringa na Kilolo kutembelea maeneo ya urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika na kuelezwa kuwepo kwa malalamiko hayo.


Pamoja na kukabidhiwa malalamiko hayo kwa maandishi,  Kitukuu huyo wa Chifu Mkwawa alipewa fursa ya kuyafafanua malalamiko hayo katika kikao kifupi kilichofanyika ndani ya ofisi za makumbusho hayo ambacho watu wengine, wakiwemo wanahabari hawakuruhusiwa kuingia.


Taarifa ya familia hiyo ilidokeza malalamiko hayo kwamba yanahusu uendelezaji wa makumbusho hayo ikiwemo ujenzi na usafi wa kaburi la chifu huyo na makaburi ya familia hiyo, ukarabati wa baadhi ya nyumba za ukoo huo zilizopo jirani na makumbusho hayo, mipaka, uendeshaji wa makumbusho na mapato yake na kukosekana kwa huduma zingine ikiwemo ya umeme na maji.


Kuhusu uendeshaji wa makumbusho hiyo, Fatuma alisema; “Makumbusho inaanza kupoteza muelekeo kwasababu wanaoisimamia na waongoza wageni sio wenyeji wa mkoa wa Iringa, hawajui mila wala utamaduni wa kabila la wahehe.”


Aidha taarifa ya familia hiyo ilidokeza kuwepo kwa kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mfanyakazi wa makumbusho hiyo inayotaka makumbusho hiyo iuzwe ili kufidia stahiki zake ambazo hakupewa baada ya kuachishwa kazi.


Akiahidi kushughulikia malalamiko hayo, Waziri Mwakyembe alisema atakutana na Waziri wa Malialisi na Utalii ambako makumbusho hiyo ipo chini yake na kuona namna ya kuyamaliza malalamiko hayo.


“Nchi hii ni yetu sote, nimechukua malalamiko hayo na nitakutana na Waziri wa Maliasili na Utalii tuangalie kwa pamoja namna ya kuyashughulikia. Naomba muwe wavumilivu na muamini kwamba serikali itayafanyia kazi,” alisema.


Awali Dk Mwakyembe alisema serikali inaendelea kuyatambua maeneo ya urithi wa ukombizi ili yalindwe na kuhifadhiwa kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadae.

 
Alisema historia ya ukombozi ina sehemu mbili, moja ikihusu bara la Afrika ambayo makao makuu yake yatajengwa jijini Dar es Salaam na ya pili ni ya ndani ambayo makao makuu yake yatakuwa Kongwa, Dodoma.


Alisema bara la Afrika linakabiliwa na tatizo kubwa sana la taarifa ya kutosha na sahihi kwasababu historia yake iliandikwa na nchi zilizotutawala na kwa kupitia mpango huo historia hiyo itaandikwa upya.


“Tarehe 29 mwezi huu mawaziri wa utamaduni wa bara zima la Afrika tutakutana Afrika Kusini chini ya mwenyekiti Tanzania na katika kikao hicho tutapannga namna ya kuanza utekelezaji wa mpango huo unaohusisha kuandikwa upya kwa historia yetu,” alisema.


Hapa nchini, Dk Mwakyembe alisema wizara yake imekwishayatambua maeneo ya urithi wa ukombozi 161 yatakayohifadhiwa kwa nguvu zote ili kulinda historia yake.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment