Saturday, 17 March 2018

MKUU WA WILAYA KILOLO AWAWEZESHA WAJASIRIAMALI ZAIDI YA 500MKUU wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdallah amewawezesha wajasiriamali zaidi ya 500 wa ukanda wa Ilula na Ruaha Mbuyuni, wilayani humo kupata mafunzo ya namna ya kuanzisha viwanda vidogo, kilimo cha mbogamboga na mbinu za kupata masoko katika kuelekea uchumi wa viwanda.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika mjini Ilula (Ilula Mtuwa) jana na juzi yalitolewa na taasisi ya Tanzania Encompass for Development Organization (TAEDO) inayotoa mafunzo ya uanzishaji wa viwanda vidogo na GBRI Business Solutions inayojishughulisha na kilimo cha mbogamboga na kuuza kwenye masoko ya ndani na nje.

Pamoja na taasisi hizo, walikuwepo pia wawakilishi wa Mradi wa Kuendeleza Wajasiriamali wa Ndani Tanzania (TLED) unaolenga kutoa elimu na fursa za kimasoko, shughuli za biashara na maarifa ya kiufundi katika biashara ndogo na za kati kupitia mafunzo na huduma za ushauri.

Akifungua mafunzo hayo, yaliyoshirikisha pia taasisi za kifedha, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Chakula na Dawa (TFDA), Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO),   Abdallah alisema mafunzo hayo ni muhimu kwasababu yatachochea maendeleo ya watu wa Kilolo kwa kuwaongezea ujuzi katika shughuli zao za uzalishaji.

“Katika maeneo mengine watu wanaoshiriki mafunzo haya wanatakiwa kulipia gharama za mafunzo, lakini mimi nimewezesha myapate bure kwa gharama ya muda na masikio yenu kwasababu nataka wilaya yangu ipige hatua stahiki katika shughuli za ujasiriamali na viwanda, kilimo chenye tija, biashara na mambo mengine yanayohusu maendeleo,” alisema.

Abdallah alisema mafunzo hayo yatasaidia pia kutatua changamoto za ajira katika wilaya na akata washiriki wasaidie kupeleka ujumbe hususani kwa vijana kwamba wanapaswa kuondokana na dhana ya kuajiriwa na badala watumie fursa zilizopo kujiajiri ili kubadili kwa haraka maisha yao, ya jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla.

“Mabilionea wengi duniani hawana historia ya kuajiriwa, walitumia maarifa kujiajiri na katika ajira zao binafsi wakaongeza ujuzi, uliongeza tija na kuwafanya leo wawe hivyo walivyo,” alisema.

Wakati huo huo mkuu wa wilaya huyo amewataka wajasiriamali hao kuzilasimisha biashara zao ili serikali kwa upande mwingine iweze kupate kodi zake stahiki ambazo ni msingi wa maendeleo mengine ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya uzalishaji na biashara na sekta zingine za kutolea huduma.

Katika mafunzo hayo, mwakilishi wa TAEDO, Kenani Kiongosi aliwafundisha kwa vitendo wajasiriamali hao namna ya kutengeza sabuni za unga na batiki na Hadija Jabiri Mkurugenzi wa GBRI Business Solutions akawapitisha kwenye hatua muhimu za uzalishaji bora wa mbogamboga na matunda kwa ajili ya matumizi mbalimbali yakiwemo ya viwandani, ndani na nje ya nchi.

Na taasisi zingine za TBS, TFDA, TCCIA, SIDO na NMB Bank zikaeleza shughuli wanazofanya na namna wajasiriamali hao wanavyoweza kutumia huduma zao katika kuboresha uzalishaji pamoja na kuzingatia taratibu zote za kisheria katika shughuli zao.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment