Tuesday, 13 March 2018

LIGANGA, MCHUCHUMA KUCHOCHEA KASI YA UCHUMI WA VIWANDAKATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof Elisante Ole Gabriel amesema ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini utapiga hatua kubwa pindi miradi mikubwa ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe itakapoanza uzalishaji.

“Viwanda haviwezi kwenda bila chuma na biashara haiwezi kuwepo bila viwanda na viwanda haviwezi kuwepo bila uwekezaji. Haya mambo matatu tunayafanyia kazi vizuri na kwa kweli tunaamini uwekezaji wa miradi hii utatutoa,” alisema juzi katika ziara yake iliyomfikisha wilayani humo kujionea maeneo ya miradi hiyo.

Profesa Gariel alisema kwa umakini mkubwa kama wizara, wanafanya kila linalowezekana ili miradi hiyo ianze kufanya kazi hatua itakayosaidia kulifikisha Taifa kwenye dhana nzuri ya Rais Dk John Magufuli ya uchumi wa viwanda.

“Watanzania waendelee kuiamini wizara kwamba miradi hii mikubwa ipo katika hatua za mwisho mwisho za kuanza utekelezaji, kama serikali tunaendelea kuchambua vizuri njia sahihi itakayokuwa na mafanikio na tija zaidi ili maamuzi ya mwisho yawe ya kimkakati  kwa faida ya kizazi hiki na kwa kizazi kijacho na kijacho,” alisema akiwataka wananchi kuwa na subira.

Alisema miradi hiyo inatekelezwa kwa ubia kati ya serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Ltd (SHG) ya China.

Awali  Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo ya Viwanda wa NDC, Dk Godwill Wanga alisema miradi ya Liganga na Mchuchuma inatekelezwa kwa mfumo unganishi wenye vipengele vitano kikiwemo cha mgodi wa chuma cha Liganga.

Alisema mgodi huo wa chuma una uwezo wa kuzalisha tani milioni 2.9 kwa mwaka huku kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma Liganga kikitarajiwa kuzalisha zaidi ya tani milioni moja kwa mwaka.

Alisema eneo lote la mgodi lina ukubwa wa kilometa za mraba 165, hata hivyo lililofanyiwa tathimini ni eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 9.7 tu linalokadiriwa kuwa na tani milioni 126 za chuma zinazoweza kutumika kwa zaidi ya miaka 100 kwa wastani wa tani milioni moja kwa mwaka.

Alisema kipengele kingine ni mgodi wa makaa ya mawe Mchuchuma wenye uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka.

“Eneo la mgodi lina ukubwa wa kilometa za mraba 140, lililofanyiwa utafiti ni kilometa za mraba 30 tu (sawa na asilimia 20) linalokadiriwa kuwa tani milioni 428 za makaa ya mawe ambayo pia yanaweza kuzalishwa na kutumika kwa zaidi ya miaka 100,” alisema.

“Kipengele kingine ni kituo cha kufua umeme cha megawati 600 huko Mchuchuma. Kati ya hizo megawati 250 zitatumika Liganga katika kuchenjua na kuzalisha chuma cha pua na megawati nyingine 350 zitaingizwa kwenye msongo wa Taifa ili kuiuzia TANESCO,” alisema.

Pia kutakuwa na njia ya msongo wa umeme wa kilowati 220 kati ya Mchuchuma na Liganga na barabara ya mkato kutoka Mchuchuma hadi Liganga.

Alisema gharama za uwekezaji katika mradi huo unganishi ni Dola bilioni tatu, ambapo dola milioni 600 ni mtaji wa muwekezaji na mkopo utakuwa dola bilioni 2.4.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Ludewa,  Andrea Tsere alimuomba Katibu Mkuu kushughulikia suala la fidia za wananchi wanaotakiwa kupisha utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kuzihusisha wizara zingine zinazohusiana na miradi hiyo ikiwemo ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano inayotakiwa kuboresha miundombinu katika miradi hiyo.

Profesa Gabriel aliahidi kurudi tena katika maeneo hayo akiwa na kamati ya bunge, mawaziri na makatibu wakuu, ambao majukumu yao yatarahisha utekelezaji wa miradi hiyo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment