Tuesday, 13 March 2018

FEED THE FUTURE YAWEZESHA HATI ZA ARDHI ZA KIMILA, IRINGA

MPANGO wa Kupunguza Njaa na Utapiamlo (Feed the Future) umewawezesha wananchi wa vijiji 18 vya wilaya ya Iringa kumilikishwa ardhi zao kisheria na kupata hati miliki za kimila za ardhi kwa kupitia Mradi wa Urasimishaji Ardhi Vijijini (LTA).

Naibu Mkurugenzi wa LTA, Malaki Msigwa alisema jumla ya hati miliki za kimila 22,231 zimetolewa kwa wananchi wa vijiji hivyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Alivitaja baadhi ya vijiji hivyo kuwa ni pamoja na Kinywang’anga, Kiponzero, Magunga, Usengelindete, Ikungwe, Malagasi, Mgama, Ilandutwa, Lwato, Udumka, Mfukulembe, Muwimbi, Makoka na Isele.

“Jumla ya vipande vya ardhi 32,141 vilipimwa katika vijiji hivyo ambavyo ni kati ya vijiji 36 vinavyotarajiwa kunufaika na mradi huu unaotekelezwa kwa miaka minne, mwaka 2016 na 2019,” alisema.

Alisema mradi wa urasimishaji ardhi unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) umelenga kuwawezesha wanavijiji kumilikishwa ardhi zao kisheria kwa kupanga matumizi bora ya ardhi ya vijijini na kutoa elimu ya sheria zinazohusu haki za ardhi.

“Mipango bora ya ardhi imekwishaandaliwa katika vijiji 29 vya mradi na kazi hiyo inaendelea katika vijiji vilivyobaki,” alisema. 

Pamoja na mradi huo kulenga kuvinufaisha vijiji 36 vya wilaya ya Iringa, Msigwa alisema mkoani Mbeya, vijiji vitano katika wilaya ya Mbeya vinatayarishiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi na kila mwenye ardhi atapimiwa na kupewa hatimiliki ya kimila.

Alisema USAID inafadhili mpango huo ili kuisaidia Tanzania kuwa na mfumo mzuri na wa wazi wa kulinda haki ya kumiliki ardhi kwa raia wote, wanaume na wanawake.

“Usajili wa ardhi ni muhimu kwasababu unaongeza ulinzi wa umiliki wa ardhi, unawezesha uwekezaji, unaongeza thamani ya ardhi na unapunguza migogoro ya ardhi,” alisema.

Alisema katika vijiji hivyo vya Iringa na Mbeya, zaidi ya hati miliki za kimila 70,000 ziatotolewa kwa wananchi wake na hivyo kusaidia kupunguza eneo kubwa la ardhi ya Tanzania ambayo haijapimwa.

Aliwataka wananchi wanaondelea kupata hati hizo kuzitumia kupata mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali za fedha ili kuchochea maendeleo yao.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment