Friday, 23 March 2018

CCM YAMBANA MCH MSIGWA SOKO KUU IRINGA, MIL 18 ZATEKELEZA AHADI YAKE
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa kimetumia zaidi ya Sh Milioni 18 katika kipindi cha wiki tatu kutekeleza ahadi ya Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka miwili tangu aitoe kwa wanajumuiya wa Soko Kuu la mjini Iringa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Katika moja ya mikutano yake ya kampeni za uchaguzi huo, Mchungaji Msigwa aliiahadi jumuiya hiyo kununua Televisheni seti za kisasa 10 zitakazofungwa katika soko hilo ili ziwawezeshe pamoja na wateja wao kufuatilia mambo mbalimbali yanayotokea ndani na nje ya nchini.

Katibu wa CCM wa Manispaa hiyo, Marko Mbanga alisema   Februari mwaka huu, CCM iliombwa kushughulikia ahadi hiyo iliyoelezwa na wana jumuiya hao kwamba inakila dalili kwamba ni hewa na kwa kuanza ilipeleka televisheni moja aina ya Sumsung  inchi 58 pamoja na king’amuzi cha Azam.

"Wakati tukikabidhi vifaa hivyo vya kutazamia matangazo ya ndani na nje ya nchi, wana jumuiya hao walituomba tuangalie uwezekano wa kuongeza Televisheni nyingine kwa kuzingatia ukubwa wa soko hilo ambalo limegawanyika sehemu mbili, la zamani na jipya," alisema.

Katika kujibu mapigo ya CCM, wiki moja baadaye (Machi 10 mwaka huu), Mchungaji Msigwa alifanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mwembetogwa mjini Iringa na kuwahahakishia wapiga kura wake kwamba ahadi aliyoitoa kwa wafanyabishara wa soko hilo ipo pale pale.

Wiki moja baada ya ahadi ya Mchungaji Msigwa waliyojiridhisha kwamba ni danganya toto, CCM walipeleka Televisheni nyingine tano aina ya Samsung, nne zikiwa za inchi 43 na moja ya Inchi 65, ving’amuzi na Sabu wufa ambazo matumizi yake katika pembe tofauti za soko hilo yalizinduliwa mapema leo na Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa Said Rubeya.

Akizindua matumizi ya televisheni hizo huku akishangiliwa na baadhi ya wafanyabiashara na wateja wa soko hilo, Rubeya alisema; “Tunampa mwezi mmoja Mchungaji Msigwa kuwaletea Televisheni nne zilizobaki katika ahadi yake ya kuleta televisheni 10, akishindwa tutajua namna ya kufanya kwasababu CCM inawapenda.”

Rubeya alisema CCM sio chama cha blabla, kinawathamini na kuwajali watanzania na katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano, kinafanya kila linalowezekana kushughulikia changamoto mbalimbali za wananachi.

Alisema kuwepo kwa luninga katika soko hilo ni jambo muhimu kwa watanzania wote wanaotumia soko hilo kutoa na kupata huduma na ndio maana CCM ikasikia kilio hicho na kukifanyia kazi kwa kasi hiyo.

Pamoja na uzinduzi wa matumizi ya televisheni hizo, Rubeya alipokea kero mbalimbali za wafanyabiashara hao na kwa niaba ya chama chake aliahidi  kuzifanyia kazi, likiwemo ombi la kuziruhusu daladala kupita katika njia za soko hilo ili kuiweka huduma hiyo ya usafiri jirani na wateja na wafanyabiashara wa soko hilo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Miyomboni lilipo soko hilo, Mahazi Hepautwa alisema atapeleka ombi katika kikao cha baraza la madiwani ili muda wakufunga  biashara katika soko hilo uongezwe kutoka saa 12.00 jioni hadi saa 4.00 usiku.

"Lengo ni kuboresha shughuli za utoaji huduma ya soko kwa wananchi. Tunataka kuona biashara katika soko hili zinakuwa kwa kuwaongezea wateja fursa ya kupata huduma zake," alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment