Wednesday, 21 March 2018

ASAS DAIRIES KUJENGA KIWANDA CHA MAZIWA TUKUYU MBEYA


KAMPUNI ya usindikaji wa maziwa ya Asas Dairies Ltd ya Mjini Iringa ipo mbioni kuanza ujenzi wa kiwanda kama hicho katika mji wa Tukuyu, wilayani Rungwe Mkoani Mbeya ikiwa ni sehemu ya mikakati yake ya kupanua shughuli zake za uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na maziwa.

 
Akizungumza na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Injia Stella Manyanya, mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Ahmed Salim Abri alisema wamepata eneo la ukubwa wa ekari mbili na nusu katika mji huo zitakazotumika kwa uwekezaji huo.
 

Injinia Manyanya alitembelea kiwanda cha Maziwa cha Asas juzi akiwa katika ziara yake mkoani Iringa kujionea shughuli za uzalishaji zinazofanywa na wawekezaji mbalimbali katika sekta ya viwanda.

Mbali na kiwanda hicho, Manyanya alitembelea pia kiwanda cha Ivori & Beverage ambao ni wazalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo pipi na chocolate Ivori,  kiwanda cha maji cha Rocks na kampuni inayojishughulisha na uzalishaji wa mbogamboga ya GBRI.Bila kutaja gharama za mradi huo mpya, Abri alisema ujenzi huo utachochea ufugaji na uzalishaji wa maziwa bora katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.


Pamoja na mpango huo, alisema kampuni yao inaendelea na upanuzi wa kiwanda cha cha Iringa utakaokwenda sambamba na matumizi ya teknolojia ya UHT inayowezesha maziwa yanayozalishwa kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika hata yasipohifadhiwa kwenye mashine za kupoozea (jokofu).

Alisema matumizi ya teknolojia hiyo ya Ultra High Temperature yatakiwezesha kiwanda chao kuongeza uzalishaji na kupanua soko lake hadi katika maeneo yasio na matumizi makubwa ya majokofu.
 

Katika hatua nyingine Abri alimwambia waziri huyo umuhimu wa kuwepo kwa sera itakayodhibiti uuzaji holela wa maziwa ili kulinda afya za walaji.
 

Alisema baadhi ya wafugaji, hasa wadogo wamekuwa wakikamua na kuuza kwa wananchi hata yale maziwa yanayokamuliwa kutoka kwa ng'ombe wenye magonjwa na walioko katika matibabu jambo ambalo ni hatari kiafya.

“Kwa kupitia sera hiyo, wafugaji walazimike kuuza maziwa yao viwandani kabla ya kufika kwa mlaji wa mwisho kwa kuwa viwanda vya maziwa vina mashine za kupima ubora wa bidhaa hiyo," alisema na kuongeza kwamba hatua hiyo itaongeza upatikanaji wa maziwa ya kutosha viwandani na kuchochea uanzishwaji wa viwanda vingi zaidi vya kusindika maziwa.
 

Wakati huo huo, Abri amemuomba waziri huyo kusaidia kuzishughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili kampuni yake na wazalishaji wengine wa viwanda vya maziwa nchini.
 
Abri alitaja Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) akisema ipo haja ya kuyaunganisha mashirika hayo kwani yamekuwa yakifanya kazi zinazofanana kwa malipo tofauti jambo linalowaongezea gharama za uendeshaji.

Pamoja na mkanganyiko huo alisema Wakala wa Vipimo kwa upande mwingi imekuwa ikifanya kazi zinazofanywa pia na TBS na TFDA kwa gharama nyingine tofauti.

 
"TFDA na TBS hawawezi kutupa vyeti vyao mpaka wamepima ujazo uliopo kwenye kifungashio cha bidhaa. Cha kushangaza tunalazimika kumlipa fedha nyingi Wakala wa Vipimo kama tozo la kupima ujazo wa bidhaa ile ile iliyopimwa na TFDA na TBS," alisema.

Mwekezaji huyo aliizungumzia pia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) akisema toka mwaka 2013 hawajapewa hati (Compliance Certificate) na kwa miaka mitatu hakuna mafunzo yoyote waliyotoa kwa watumishi wao, pamoja na kutakiwa kulipa Sh 750,000 kila mwaka kwa ajili ya watimishi watatu.

Naibu Waziri aliipongeza kampuni hiyo kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazozidi kujipatia soko kubwa  ndani na nje ya nchi huku akiahidi kushughulikia changamoto zilizotajwa.

"Nimepokea changamoto hizi, nazichukua kama zilivyo na niahidi tutazifanyia kazi kwa kuwa kama serikali ni wajibu wetu kuwasikiliza wawekezaji wetu, kuwalinda na kushughulikia changamoto zao kwa kuzingatia maslai mapana ya Taifa," alisema.

Pamoja na kuzichukua changamoto hizo, Injinia Manyanya alisema serikali imeanza kulifanyia kazi wazo la kuwa na mwavuli mmoja utakaofanya kazi kwa niaba ya TBS na TFDA.


 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment