Wednesday, 21 February 2018

SERIKALI YABAINI UDANGANYIFU WA MAPATO MGODI WA DHAHABU NYAKAVANGALA


SERIKALI imebaini udanganyifu mkubwa wa wastani wa kiwango cha dhahabu kinachozalishwa katika mgodi wa dhahabu wa Nyakavangala wilayani Iringa na kuagiza wataalamu wake wakokotoe kiasi cha fedha  ambacho serikali imekuwa ikiibiwa kupitia mrabaha wake ili wamiliki wa mgodi huo walazimishwe kulipa. 

Mgodi huo  uliopo katika kijiji cha Nyakavangala, kata ya Malengamakali tarafa ya Isimani ulikabidhiwa na kijiji hicho kwa Thomas Masuka kama msimamizi mkuu wa mgodi na wenzake wengine 19 Mei mwaka jana ili kuondokana na uchimbaji holela, wakati taratibu zingine za kupata leseni zikiendelea.

Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko alipokuwa akizungumza na wachimbaji na viongozi wa mgodi huo uliofungwa hivikaribuni baada ya kutokea maafa yaliyohusisha baadhi ya wachimbaji hao kufukiwa wakati wakiwa katika shughuli ya uchimbaji na wengine kufariki dunia.

Akiagiza mgodi huo ufunguliwe katika kipindi cha wiki mbili zijazo baada ya changamoto zake zote kushughulikiwa, Biteko alisema taarifa ya wachimbaji hao ilikuwa ikionesha kila kiroba cha mchanga wa dhahabu kilikuwa kikitoa wastani wa gramu 0.28 ya dhahabu, lakini wataalamu wa wizara walipokwenda kupima ilibainika kila kiroba kimekuwa kikitoa wastani gramu 2.5 ya dhahabu.

“Acheni kuidanganya serikali, mnapofanya kazi zenu hakikisheni serikali inapata kinachoihusu ili iweze kuwahudumia ninyi na wengine kwa kupitia huduma mbalimbali inazotoa kama barabara, maji, afya, elimu na nyinginezo” alisema..

Alisema baada ya kubaini udanganyifu huo,  serikali itaunda timu kungalia kiasi cha mrabaha uliopotea na namna wamiliki wa mgodi huo watakavyotakiwa kulipa.

“Yako mambo yanayosameheka, lakini sio hela ya serikali, naomba msiniponze mimi na waziri wangu, katika hili hakuna msamaha na mnajua mwenye wajibu wa kutoa msamaha yupo kwa mujibu wa sheria kwahiyo maagizo yangu mtalazimika kulipa kiasi chote kitakachobainika mlikwepa kuilipa serikali,” alisema.

Awali Meneja wa mgodi huo, John Denis alisema tangu mgodi huo uanze kuzalisha dhahabu Mei, mwaka jana, jumla ya viroba 21,150 vya mchanga wa dhahabu vimezalishwa hadi ilipofika Desemba mwaka jana.

Denis alisema asilimia 20 ya viroba hivyo vilitolewa kwa wafanyakazi wanaosimamia mgodi, serikali ya kijiji na halmashauri ya wilaya ya Iringa huku vingine 932 vikitolewa kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kituo cha afya Mkulula.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Iringa, Robert Masunya alisema kwa kupitia mgao huo, halmashauri yake ilipata Sh Milioni 17.1, kijiji cha Nyakavangala Sh Milioni 36.8 na kituo cha afya Mkulula kilichangiwa Sh Milioni 64.9.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewataka wachimbaji wa madini katika mgodi huo kufanya kazi hiyo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji wa madini huku akihimiza kodi zote stahiki zinazotakiwa kulipwa serikalini zitolewe na kwa wakati


Reactions:

0 comments:

Post a Comment