Thursday, 1 February 2018

MTANDAO UNAOTAFITI KERO ZA BIASHARA WATAJA VIKWAZO VIPYA VYA BIASHARA NCHINI


MTANDAO Unaotafiti Kero za Kibiashara Nchini (Multi Actors Intergration-MAI) umevitaja vikwazo vipya vinavyoikumba sekta ya biashara nchini na kuwataka wajasiriamali kuzitumia taasisi za fedha kupata mikopo itakayoongeza mitaji katika shughuli zao.

Akifungua kikao kazi cha mtandao huo jana mjini Iringa Mwenyekiti wa MAI, Lucas Mwakabungu alisema baadhi ya wajasiriamali wamekuwa waoga kuongeza mitaji ya biashara zao na wengine wamefunga biashara hizo wakilalamika kupungua kwa mzunguko wa fedha mitaani.

“Lakini pia zipo baadhi ya taasisi za fedha zinazolalamikiwa kwa muda mrefu sasa kusita kuwakopesha wajasiriamali na wakati huo huo zimeongeza masharti ya mikopo; yanayolalamikiwa kuwa magumu,” alisema.

Akitoa mfano Mwakabungu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Iringa alisema pamoja na kukidhi masharti mengi ya kibenki, wapo wakulima waliokosa mikopo ya kilimo kutoka katika moja ya benki za biashara nchini (hakuitaja jina) kwasababu walishindwa kuwasilisha mkataba wa ununuzi wa bidhaa wanazozalisha kutoka kwa wateja wao.

“Changamoto nyingine ambayo tumeikuta kwa wazalishaji wa mafuta ya alizeti ambao wanalalamika kushindwa kukuza viwanda vyao kwasababu ya kodi nyingi, usajili wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na namna ya kuihamishia serikalini kodi hiyo,” alisema.

Alisema kwa kupitia program ya BEST inayojishughulisha na uboreshaji wa mazingira ya biashara Tanzania, MAI imekuwa ikiutumia Umoja wa Vyuo Vikuu Nchini ambao ni mwanachama wake kufanya tafiti mbalimbali katika sekta hiyo, na baadaye kutoa ushauri kwa serikali na wadau wake wa namna kero hizo zinavyoweza kushughulikiwa kwa maslai ya pande zote mbili.

 “Kwahiyo kwa siku mbili tulizokutana Iringa tulikuwa tunapitia baadhi ya vikwazo vilivyojitokeza kati ya Julai na Desemba mwaka jana, na tumekuja na ushauri wa namna vikwazo hivyo vinavyoweza kufanyiwa kazi,” alisema.

Alisema MAI inaundwa na wadau wa sekta ya biashara wa mikoa ya Iringa, Morogoro, Mbeya, Njombe na Ruvuma ambayo ipo katika Ukanda wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), ikiwakilishwa na chemba za TCCIA.

Wadau wengine wa MAI ni Umoja wa Vyuo Vikuu Nchini, vyombo vya habari na washirika wengine katika sekta ya biashara na kilimo likiwemo Jukwaa la Wadau wa Kilimo Tanzania (ANSAF), taasisi inayojihusisha na kilimo cha mbogamboga, matunda na maua nchini (TAHA) na mpango wa SAGCOT wenyewe.

Awali Mratibuwa Umoja wa Vyuo Vikuu Nchini, Dk Mariam Nchimbi alisema ndani ya MAI umoja huo unafanya kazi ya kuwasaidia wafanyabiashara kufanya tafiti za kero zao.

“Kwahiyo tunapokea malalamiko mengi ya wafanyabishara, kwa kutumia ujuzi wetu tunafanya utafiti ili kuelewa zaidi kero zao, maana wakati mwingine wanaweza kulalamika lakini malalamiko yao yasiwe tatizo,” alisema

Reactions:

0 comments:

Post a Comment