Sunday, 11 February 2018

MAKAMU WA RAIS, MNEC ASAS WACHANGIA SEKTA YA ELIMU KILOLO

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (MNEC-CCM) anayewakilisha mkoa wa Iringa, Salim Abri Asas wametoa michango ya fedha na vifaa vya ujenzi kuunga mkono juhudi za kuboresha sekta ya elimu zinazofanywa katika wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Wakati makamu wa Rais ametoa mchango wa Sh Milioni tano kusaidia juhudi hizo, MNEC Asas amechangia bati 500 na mifuko 300 ya saruji.

Katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa wazi wa mji wa Ilula, wilayani humo juzi, makamu wa rais aliipongeza halmashauri ya wilaya hiyo kwa kupata hati.

“Lakini pia niwapongeze viongozi wa wilaya hii, wananchi na wadau wake wa maendeleo kwa ujumla kwa namna mnavyoonesha juhudi katika shughuli zenu mbalimbali za maendeleo,” alisema huku akigusia sekta mbalimbali za maendeleo kama kilimo na viwanda.

Na akampongeza Asas na kampuni yake ya Asas Group kwa namna inavyochangia shughuli mbalimbali za maendeleo mkoani Iringa huku akiwataka wadau wengine waunge mkono jitihada hizo.

Kiongozi huyo alizungumzia pia makusanyo ya halmashauri hiyo akisema yanaonesha dalili njema na akataka juhudi zaidi ziongezwe katika vyanzo vyote vinavyopaswa kulipiwa.

Alizitaka mamlaka zinazohusika kutowanyanyasa wananchi kwa kuwalazimisha kulipia kodi, bidhaa ambazo hazistahili kulipiwa.

“Nilipokuwa makao makuu ya wilaya yenu, nimeambiwa katika baadhi ya maeneo wananchi wanatozwa ushuru wa mbao na kuni wanazokusanya kwa ajili ya matumizi yao mamumbani, hiyo sio sahihi kwa kuwa sio za biashara,” alisema.

Kuhusu kero ya maji katika mji huo wa Ilula alisema serikali inaendelea kuifanyia kazi changamoto hiyo, mpango ukiwa ni kuimaliza kabisa ili wananchi wote wa mji huo wafikiwe na huduma ya maji safi na salama.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameipongeza wilaya ya Kilolo kwa kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi na kuagiza zoezi la upimaji wa vijiji kuendelea ili kuondoa migogoro ya ardhi kati ya kijiji na kijiji.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment