Monday, 26 February 2018

MAHAMUDU MGIMWA ATOA MSAADA WA MAMILIONI JIMBONI MWAKE


MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahamudu Mgimwa ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 12 vitakavyotumika kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu na afya jimboni humo.

Kati ya vifaa hivyo, yapo mabati 280, mifuko 310 ya saruji, rangi za maji na mafuta na sim tenki za kuhifadhia maji.

Akikabidhi vifaa hivyo jana, Mgimwa alisema vijiji vinavyonufaika na msaada huo ni vya kata ya Mapanda, Kibengu, Ihanu na Sadani.

“Nilifanya ziara katika vijiji vya kata hizo, nikaona wananchi wanavyojitoa kuboresha  sekta ya elimu na mimi kama mbunge wao nikaamua kuwaunga mkono kwa kuchangia vifaa hivyo,” alisema.

Alivitaja vijiji vinavyonufaika na msaada huo kuwa ni pamoja na Ihimbo, Ukami na Chogo katika kata ya Mapanda; na Kipanga, Igeleke, Kibengu, Usokami na Igomtwa katika kata ya Kibengu.

Vingine ni kijiji cha Lulanda katika kata ya Ihanu na katika kata ya Sadani Mgimwa sehemu ya msaada huo inakwenda kusaidia ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari Mgalo.

Mmoja wa wanufaika wa msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Isupilo, Onorata Mwanuke alisema kwa msaada waliopatapata wanakwenda kukamilisha ujenzi wa nyumba moja ya mwalimu.

“Mahitaji ya nyumba za walimu ni tisa, zilizopo ni tatu na mbunge ametoa msaada wa mifuko 30 ya saruji kusaidia kukamilisha nyumba ya nne ya mwalimu. Tunategemea mbunge ataendelea kutuunga mkono,” alisema.

Kwa niaba ya vijiji vyote vilivyonufaika na msaada huo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Asheri Mtono alishukuru akisema; “halmashauri hii ina changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu ya shule na kwa msaada huu wa mbunge mazingira hayo yatakwenda kuboreshwa.”

Mtono ambaye pia ni diwani wa kata ya sadani alisema pamoja na mchango wa mbunge huo na wadau wao wengine, wananchi wa vijiji hivyo na vingine vyote katika halmashauri hiyo wanahitajika kuendelea kuchangia shughuli zao za maendeleo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment