Saturday, 10 February 2018

IVORI WAFIKISHA KILIO CHA SUKARI YA VIWANDANI KWA MAKAMU RAISKIWANDA cha Ivori & Beverage cha mjini Iringa ambao ni wazalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo pipi na chocolate maarufu za Ivori kimepeleka kwa Makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan kilio chake kinachohusu urasimu wa utoaji wa vibali vya kuagiza nje ya nchi sukari ya viwandani inayotumika kuzalisha bidhaa hizo.

Makamu wa Rais alitembelea kiwanda hicho jana katika muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Iringa kujionea shughuli mbalimbali za maendeleo  zinazofanywa na wakazi wa mkoa huo.

Akizungumzia changamoto za kiwanda mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho,  Suhail Esmail Thakore alisema upatikanaji wa vibali vya kuagiza sukari hiyo ni moja ya changamoto kubwa inayokikabili kiwanda chao.

Thakore alisema kwa mwaka wa fedha 2017/2018 mahitaji yao ni tani 3,000 lakini walizoruhusiwa kuingiza nchini hadi sasa ni tani 848 hali inayotishia uzalishaji kama huko mbele vibali vingine havitatolewa.

“Januari mwaka huu ilipita timu ya uhakiki na hadi sasa hakuna majibu yoyote juu ya utoaji wa vibali vingine jambo linalotuyumbisha na kutukosesha muelekeo kwani huko mbele kuna hatari ya kusimamisha uzalishaji kama hatutapa sukari hiyo,” alisema.

Alisema mahitaji ya sukari hiyo yanaongezeka kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji unaochochewa na ukuaji wa soko ambalo awali lilikuwa gumu kwao kwani baadhi ya bidhaa kama zao zilikuwa zinaingizwa nchini kwa wingi na kuuzwa kwa bei ndogo zaidi kwasababu kulikuwa na mianya ya ukwepaji wa kodi.

“Baada ya  serikali ya a wamu ya  tano chini ya Rais Dk  John  Magufuli   kuingia madarakani  soko la ndani   linazidi kukua hiyo ikitokana na kubanwa kwa mianya na njia  za   kukwepa ushuru wa bandarini na hivyo kukuza soko la bidhaa za ndani,” alisema

Aliiomba serikali kusikia   kilio   chao   kwa kutafuta  ufumbuzi wa  haraka wa  jambo hilo zito akisema bodi ya sukari inatakiwa kutoa muongozo ili kutoathiri uzalishaji wao.

Akitoa  taarifa  ya  kiwanda hicho, Thakore alisema mbali na pipi na chocolate kiwanda hicho kilichoanzishchwa mwaka 2007 kinajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali Cocoa Powder, Tomato na Chill Sauce.

“Bidhaa zetu zote na hasa pipi na cocoa powder zinashindana vizuri sana katika soko la nje na bidhaa za aina hiyo zinazozalishwa katika nchi nyingine nyingi ikiwemo Kenya,” alisema na kutaja baadhi ya masoko ya nje ya bidhaa zao kuwa Kenya yenyewe, Uganda, Msumbuji, Burudi na Jamuhuri ya Demokrasia ya Congo.

Akizungumzia maendeleo ya kiwanda hicho, Thakore alisema kimepitia hatua mbalimbali za mapinduzi yake toka kiwanda kidogo hadi ukubwa kilionao sasa huku kikiwa kimeajiri watu 150, kati yao 105 wakiwa na ajira za kudumu.

“Pia  kiwanda hiki kimeweza kuzaa kiwanda kingine cha pipi  ambacho ujenzi wake upo katika hatua za mwisho kukamilika na ni matarajio yetu katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne ijayo kitaanza uzalishaji jambo litakaloongeza mahitaji ya sukari hiyo,” alisema huku na kuongeza kwamba kiwanda hicho kipya kitatoa ajira kwa watanzania zaidi ya 60.

Alisema  sehemu kubwa ya malighafi zinazotumika kwa uzalishaji zinazalishwa nchini ikiwemo Cocoa toka wilayani Kyela mkoani Mbeya, nyanya toka Ilula wilayani Kilolo mkoani Iringa na mahindi ya Iringa, Ruvuma na Rukwa.

Makamu wa Rais amesifu bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho akisema ubora wake umezifanya zipenye kirahisi katika soko la kimataifa na kuleta ushindani unaoliletea Taifa sifa.

Makamu wa Rais alisema dhamira ya kampuni inayomiliki kiwanda hicho, uwekezaji mkubwa na matumizi ya teknolojia ya kisasa yamekifanya kiwanda hicho kipate mafanikio hayo yanayochagiza vyema mapinduzi ya serikali ya viwanda nchini.

Alisema Taifa linapaswa kujivunia kuwa na kiwanda kama hicho na ambacho bidhaa zake zinaleta ushindani mkubwa kwa soko la kimataifa huku akiwataka wawekezaji wengine ambao hawajafikia kiwango hicho kuwa na malengo hayo.

“Ndugu  zangu, muelekeo wa Taifa letu ni Tanzania   ya   viwanda, tunataka kujenga uchumi  mpya  katika  nchi  yetu; tukiwa na  viwanda vingi kama    hivi   basi   uchumi wetu ukuwa zaidi na zaidi na hivyo kuleta mafanikio makubwa kwa Taifa na watu wake kwani mbali na ajira za moja kwa moja utachochea uzalishaji wa rasilimali zinazotumiwa kiwandani hapa,” alisema.

Kwa upande wa serikali alisema wanaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na akaahidi kuzishughulikia changamoto zinazokwamisha au kutaka kuzorotesha uwekezaji na kwa upande wa wananchi akawataka kudumisha amani iliyopo akisisitiza hiyo ndiyo nguzo ya uchumi imara.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment