Monday, 5 February 2018

DC KASESELA, HALMASHAURI WAHAHA KUMSAIDIA MUWEKEZAJ


MKUU wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela na halmashauri ya wilaya hiyo kwa pamoja wanahaha kufanikisha uwekezaji wa kiwanda kikubwa cha kusindika nyama na maziwa katika kijiji cha Kidamali waliosema unakwamishwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Mwekezaji huyo kutoka Dubai, Shafa Farms Ltd atakayetumia majengo ya kilichokuwa kiwanda cha Sigara aina Nyati, amekwishaanza taratibu za awali za uwekezaji lakini Tanesco wanakataa kumpatia huduma hiyo.

“Tanesco hawataki kumpa umeme mwekezaji huyu kwasababu aliyekuwa mmiliki wa kiwanda hicho cha Sigara anadaiwa zaidi ya Sh Bilioni 2 na shirika hilo,” alisema Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Steven Mhapa juzi wakati halmashauri hiyo ikizindua mkakati wake wa uanzishwaji viwanda vipya.

Ifikapo Desemba 31, mwaka huu halmashauri hiyo inatakiwa kuwa na viwanda vipya 35 kati ya viwanda 100 vinavyotakiwa kujengwa mkoani Iringa katika kipindi hicho ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk John Magufuli linalotaka kila mkoa ujenge viwanda vipya 100.

Akiwaita Tanesco ni kikwazo kwa uwekezaji huo, Mhapa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa (ALAT) alisema halmashauri yake inataka kupoteza fursa hiyo kwasababu mwekezaji huyo anataka kutumia majengo yaliyokuwa na deni la mwekezaji wa zamani.

“Deni sio la mwekezaji huyu, deni ni la kiwanda cha Nyati ambacho hakipo tena baada kusitisha uzalishaji na kuuza mitambo yake. Kwahiyo ananyimwa huduma kwasababu hiyo,” alisema na kuzungumzia faida za kiuchumi ambazo wilaya, mkoa na Taifa watapata endapo kiwanda hicho ambacho soko lake kubwa litakuwa nje ya nchi, kitafunguliwa.

Mhapa alisema serikali ya awamu ya tano inataka nchi ya viwanda, na ili mpango huo uweze kufanikiwa ni lazima urasimu uliopo kwenye baadhi ya taasisi za serikali uondolewe na mazingira mazuri ya uwekezaji zikiwemo huduma za maji, barabara na umeme yawekwe.

Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela alisema sekta ya viwanda ndio sekta inayoweza kulikomboa Taifa na akawataka wadau kuzingatia maelekezo ya serikali ili kufanikisha azma ya nchi ya viwanda.

“Mwalimu Nyerere aliweka viwanda katika kila mkoa, vingi vikafa na kwa muda mrefu maendeleo ya sekta hiyo yalikuwa ya kusuasua. Kaja Dk Magufuli anatuongoza kurudisha azma ya nchi ya viwanda,” alisema.

Alisema katika halmashauri ya wilaya ya Iringa kuna viwanda vidogo 295, vya kati 10 na vikubwa vinne ambavyo kwa pamoja vimetoa ajira ya moja kwa moja watu 456.

Akizungumzia suala la mwekezaji huyo, Kasesela aliiagiza Tanesco waache urasimu huo na wafunge umeme katika kiwanda hicho kipya ili taratibu za zingine ziendelee.

“Tanesco wakiendelea kukaidi, nitawashitaki kwa Rais kwani wanachofanya ni kuzuia uwekezaji wa viwanda 35 katika halmashauri yangu,” alisema.

Akizundua mkakati wa viwanda katika halmashauri hiyo, Kasesela alisema halmashauri imetenga maeneo mengi kwa ajili ya uwekezaji zikiwemo ekari 10 katika kijiji cha Kalenga, ekari 50 Ugwachanya, Ekari 10 Ihemi, ekari 50 Tungamalnega na ekari 20 Nduli mpakani na mengine mengi yanaendelea kupimwa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment