Wednesday, 28 February 2018

CCM WATUMIA SAA 24 KUTEKELEZA AHADI YA MIAKA 2 YA MBUNGE MSIGWA
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini kimetoa msaada wa Televisheni moja aina ya Sumsung Inchi 58 na king’amuzi cha Azam chenye malipo ya mwezi mmoja kwa jumuiya ya wafanyabiashara wa soko kuu la mjini Iringa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyoshindwa kutekelezwa na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kwa mwaka wa pili sasa tangu aitoe wakati wa kampeni zake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mchungaji Msigwa anayeongoza jimbo hilo kwa awamu ya pili sasa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amelalamikiwa na wafanyabiashara hao kupiga danada kuitekeleza ahadi hiyo iliyotekelezwa na CCM mapema leo, baada ya jana kupewa taarifa hiyo.

Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa hivyo, Mwenyekiti wa CCM Iringa Mjini, Said Rubeya alisema; “baada ya kusikia kilio chenu kwamba mliahidiwa na hamjatekelezewa, tumeamua kutekeleza.”

Huku akishangiliwa na baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo, Rubeya alisema mapema jana alikutana na mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo, akasikiliza kilio hicho na leo wametekeleza wakiongozwa na falsafa ya Rais Dk John Magufuli ya Hapa Kazi Tu.

“Tulipoletewa ombi hili hatujachukua miaka miwili kama mwenzetu wa Chadema, sisi kama CCM tumeona tuje tulekeze Ilani ya chama chetu kwa vitendo kwasababu tunaamini juu ya kutenda, sisi sio jamii ya walalamishi wanaoamini kulalamika ndio suluhu ya kutatua jambo, sisi tunaamini juu ya kufanya kazi,” alisema akikabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 2.

Akipokea msaada huo na kushukuru kwa niaba ya wafanyabiashara hao katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati (CCM) na viongozi na wapenzi wa chama hicho, mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo, Anold Fusi aliahidi kuvitunza vifaa hivyo kwa manufaa ya jamii hiyo.

“Pamoja na msaada huu tunaomba pia mtusaidie televisheni nyingine ndogo ndogo zitakazofungwa kwenye baadhi ya kona za soko hili kwa kuwa soko ni kubwa na huduma hii inahitajika sana,” alisema huku Rubeya akiipokea ahadi hiyo na kuahidi kuifanyia kazi.

Baadhi ya wafanyabiashara na wateja wa soko hilo walioongea na mtandao huu hii leo wameipongeza CCM kwa namna inavyosikiliza changamoto za wananchi na namna inavyozishughulikia.

 “Kwa kweli tulikatishwa tamaa na ahadi ya Mchungaji Msigwa, maana ni muda mrefu toka aitoe lakini kumekuwa hakuna utekelezaji pamoja na uongozi wetu kujitahidi kumkumbusha mara kwa mara,” alisema mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Grace Pangani.

Naye Christopher Mgeni alisema wamefurahishwa na msaada huo wakisema umekuja katika kipindi muafaka ambacho timu yao ya Lipuli FC inayoshiriki ligi kuu Tanzania Bara, michezo yake pia inarushwa katika king’amuzi cha Azam.


“Hii itatuwezesha kufuatilia kwa karibu mechi zote za Lipuli kupitia king’amuzi hiki, lakini tutapata uhondo wa matukio mengine mbalimbali wakati tunaendelea na biashara zetu,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment