Monday, 5 February 2018

BILIONI 5.2 ZA UMOJA WA ULAYA ZAWAFUATA WAKULIMA WA MPUNGA IRINGAUMOJA wa Ulaya (EU) umetoa zaidi ya Sh Bilioni 5. 2 kuliwezesha Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wakulima wa mpunga wa wilaya ya Iringa kutunza zao hilo baada ya mavuno; ili kuepuka hasara na kumudu ushindani wa biashara.

Uzinduzi wa mradi huo utakaowanufaishwa zaidi ya wakulima 10,000 ulifanyika juzi mjini Iringa katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa vijiji vinavyolima zao hilo wilayani humo, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, wawakilishi wa wizara, mkuu wa wilaya ya Iringa, madiwani na wadau wengine wa zao hilo.

Akiuzindua, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema usalama wa chakula ni jambo linalopewa kipaumbele na serikali na kwasababu hiyo wadau mbalimbali wamekuwa wakishirikishwa kutekeleza mikakati na program mbalimbali zenye nia ya kuboresha kilimo na uzalishaji wa chakula nchini.

Alisema umuhimu wa zao la mpunga katika kuhakikisha kunakuwepo na uhakika wa chakula hauwezi kupuuzwa kwani mchele ni moja ya chakula kikuu nchini na watu wengi mijini na vijiji wanategemea mpunga kama zao la chakula na pia chanzo cha ajira na kipato.

Alisema tatizo la upotevu na uharibifu wa zao hilo ni kubwa kutokana na mbinu duni za uvunaji, ukaushaji, usafirishaji, uhifadhi na usindikaji.

Masenza aliipongeza EU kwa msaada huo na akawataka FAO  ambao ni watakelezaji wakuu wa mradi na Taasisi ya Maendeleo Mjini na Vijijini (RUDI) ambaye ni mtekelezaji mwenza wa mradi kufanikisha malengo ya mradi.

Awali mwakilishi wa EU, Liesl Karen Inglis alisema umoja huo utaendelea kusaidia sekta ya kilimo kama moja ya maeneo yake ya kipaumbele nchini  kupitia Mfuko wake wa Maendeleo (EDF) ulioanza mwaka 2014 na utakaodumu hadi 2020.

“Kilimo ni ufunguo wa maendeleo ya Tanzania na kinatoa fursa kubwa katika kukuza mahusiano yake na Umoja wa Ulaya,” alisema.

Pamoja na kwamba mchele chakula kikuu na matumizi yake yanazidi kuongezeka,  Tanzania imeendelea kuagiza mchele mwingi kutoka nje ya nchi kwasababu kilimo cha zao lake (mpunga) kinakabiliwa na  ya changamoto mbalimbali mbali ukiwemo uzalishaji mdogo.

 “Ushindani wa kibiashara wa mchele wa Tanzania unaathiriwa na uzalishaji mdogo kwasababu unategemea zaidi mvua, upatikanaji na matumizi hafifu ya mbegu bora, kilimo cha kienyeji na miundombinu hafifu ya umwagiliaji,” alisema.

Akitoa takwimu za upotevu wa zao hilo, alisema utafiti unaonesha asilimia 15 hadi 25 ya punje za mchele hupotea wakati wa mavuno na asilimia 25 hadi 50 hupotea wakati wa ukaushaji, usafirishaji, uhifadhi, usindikaji na wakati wa matumizi yake.

Mwakilishi wa FAO nchini, Fred Kafeero alisema uzalishaji wa mpunga unahitaji mbinu za utunzaji sahihi wa mazao baada ya mavuno ili kuepuka hasara na ufikiaji wa masoko yenye faida lazima uboreshwe ili wakulima wafaidike na juhudi zao.

Alisema kwa kupitia mradi huo wataimarisha daraja kati ya wadau wa kuongeza thamani ya mazao kwa kujumuisha wanunuzi kutoka sekta binafsi na umma kwa kupitia mbinu jumuishi za biashara.


“Afua hizi zinategemewa kuleta ujuzi wa kiufundi na utawala ambao ni muhimu kwa wakulima wadogo wanaojihusisha na kilimo cha mpunga ili kukuza uwezo wao kiushindani,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment