Thursday, 1 February 2018

BILIONI 3.7 KUJENGA SOKO LA KISASA MJINI IRINGA


BENKI ya Dunia imetoa zaidi ya Sh Bilioni 3.7 kwa halmashauri ya manispaa ya Iringa zitakazotumika kujenga soko la kisasa litakalokuwa na  ghorofa moja.

Soko la Mlandege (Maarufu kama Soko Mjinga) limevunjwa pamoja na vibanda vyake vyote kupisha ujenzi huo unaotarajiwa kuanza wiki mbili zijazo na kukamilika katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe, kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Omary Mkangama na kampuni ya Home Africa Investment Corporation Ltd ya jijini Dar es Salaam iliyoshinda tenda ya ujenzi wa soko hili walitiliana saini ya makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo juzi.


Akizungumzia mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela aliipongeza halmashauri hiyo kwa kubuni na hatimaye kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo aliosema utakaboresha zaidi mandhari ya mji wa Iringa.

Kasesela alitoa onyo kwa mkandarasi huyo akisema anatakiwa kujenga mradi huo kwa kuzingatia ubora unaotakiwa na endapo atakwenda kinyume hawatasita kumnyang’anya kandarasi hiyo.

“Na niwahakikishie wananchi wote waliokuwa wakifanya bishara zao katika soko la zamani, haki yao haitapotea, wote watapata nafasi,” alisema.

Aliwaomba wafanyabishara hao kwenda kwa diwani wa kata ya Mlandege na kuorodhesha majina yao ili kuweka kumbukumbu zao sawa.

Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni hiyo, Shukuru Kavenuke alisema kampuni yao inauzofu wa kimataifa katika ujenzi wa majengo makubwa, kwahiyo ina hakika ya kuifanya kazi hiyo kwa ubora na kwa muda uliopangwa.

Wakati huo huo, mkuu wa wilaya alisema halmashauri ya manispaa hiyo imepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kilometa moja kwa kiwango cha lami.

“Barabara hizi sasa zinajengwa kwa kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini yaani TARURA. Na tumekubaliana kwa kupitia fedha hizo tujenge barabara ya Mtwivila darajani kwa kiwango hicho,” alisema

Reactions:

0 comments:

Post a Comment