Wednesday, 21 February 2018

BAADA YA KUJIVUA UNAIBU MEYA, IGOGO AINYONG'ONYEZA ZAIDI CHADEMA

Image result for daddy igogo


NGUVU ya kisiasa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika jimbo la Iringa Mjini linaloongozwa na mbunge na meya kutoka chama hicho inazidi kunyong’onyea baada ya diwani wa kata ya Gangilonga ambaye pia ni naibu meya wa manispaa hiyo kutangaza kuachia nyadhifa hizo.

Igogo aliyekuwa mmoja kati ya madiwani wachache wasomi wa chama hicho na ambaye pia ni mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCU) cha mjini Iringa alisema ameachia ngazi nafasi hizo kwasababu zilizo ndani ya moyo wake.

Akizungumza na mtandao huu leo, Igogo alisema; “Nimeamua kuwa raia wa kawaida na ninawashukuru wana Gangilonga kwa kuwa na mimi katika kipindi kigumu nilichopita katika siasa.”

Alipotakiwa atoe ufafanuzi wa sababu zilizopo ndani ya moyo wake na kipindi kigumu alichopita katika siasa alisema hana cha kufafanua japokuwa maamuzi hayo ni kwa faida ya maisha yake ambayo pia hakuyafafanua.

Kujitoa kwa Igogo kunafanya chama hicho kipoteze jumla ya madiwani 10 ndani ya miezi mitano illiyopita ambao kati yao saba ni wa kuchaguliwa na watatu wa viti maalumu.

Wakati madiwani wengine waliojiengua wakijiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), Igogo alisema ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Chadema na mjumbe wa kamati kuu ya wilaya ya chama hicho.

“Nabaki kuwa mwanachama na kiongozi wa chama. Nilichojivua ni udiwani na nafasi ya unaibu meya katika baraza la madiwani la manispaa ya Iringa,” alisema.

Kujiondoa kwa madiwani hao kunaifanya Chadema iliyonyakua viti 14 kati ya 18 vya udiwani katika jimbo hilo mwaka 2015 na kufanikiwa kubeba halmashauri hiyo, kubakiwa na madiwani saba ikiwa ni miaka mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa 2020.

Wakati Chadema ikibakiwa na madiwani saba wa kuchaguliwa, CCM kwa upande wake kimeongeza idadi ya madiwani kutoka wanne hadi sita baada ya kata mbili kufanya uchaguzi mdogo na inaendelea kujipanga kushinda chaguzi ndogo katika kata tano zilizo wazi.


Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe hawakupatikana kuzungumzia maamuzi ya diwani huyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment