Monday, 22 January 2018

WANA KILOLO WA DAR MORO WACHANGIA SEKTA YA ELIMU KILOLO
ZAIDI ya Sh Milioni 16 zimechangwa na wana Kilolo waishio Dar es Salaam na Morogoro kuunga mkono harakati za Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah zinazolenga kuwawezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari mwaka huu kupata nafasi hiyo ifikapo Machi, mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Aloyce Kwezi inaonesha jumla ya wanafunzi 4,289 wamechaguliwa kujiunga na shule za kutwa na bweni katika wilaya hiyo, mwaka huu.

Kutokana na ongezeko la wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na elimu hiyo, Kwezi alisema halmashauri hiyo imejikuta na upungufu wa vyumba vya madarasa 46 vinavyotakiwa kujengwa na kukamilishwa mapema iwezekanavyo.

“Tunaendelea kukamilisha ujenzi wa miundombinu hasa vyumba vya madarasa ili wanafunzi wote waliochaguliwa wapate nafasi katika shule walizochaguliwa ifikapo Machi mwaka huu,” mkuu wa wilaya alisema hivikaribuni mjini Morogoro wakati akiendesha harambee ya kuchangia ujenzi huo baada ya kufanya nyingine Dar es Salaam.

Wakati wana Kilolo zaidi ya 200 walishiriki harambee ya jijini Dar es Salaam na kuchangia zaidi ya Sh Milioni nane; wana Kilolo 30 wa mjini Morogoro nao walichanga zaidi ya Sh Milioni nane.

Mkuu wa wilaya alisema fedha hizo zinatumika kununua sementi, mabati na vifaa vingine vya ujenzi ili kuwezesha vyumba hivyo vya madarasa ambavyo ujenzi wake una mchango wa wananchi wa maeneo husika ya wilaya hiyo, kukamilika ndani ya muda.

“Niwashukuru sana wana Kilolo wa mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro kwa michango yao hii na tumepokea ahadi zao za kuendelea kuchangia maendeleo ya wilaya yao kwa utaratibu wa kila mwaka,” alisema.

Alisema wilaya hiyo inaendelea kufanya maandalizi ya kukutana na wana Kilolo na marafiki wa wilaya hiyo waishio mjini Iringa na Dodoma kupitia mkakati wa kuwahamasisha kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.

Pamoja na kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo, Abdallah alisema; “Kwa kupitia mikutano hii ya harambee, tunawahamasisha wana Kilolo na wadau wengine kurudi na kuja wilayani kwetu kwa lengo la kuwekeza.”


Alisema wilaya hiyo ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya kilimo, utalii na ina ardhi ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na miradi mingine ya maendeleo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment