Sunday, 7 January 2018

SIKU ZA MSTAHIKI MEYA WA MANISPAA WA IRINGA KUENDELEA KUKALIA KITI HICHO ZAHESABIKA

Image result for alex kimbe

SIKU za Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe kuendelea kukalia kiti hicho kupitia chama chake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zinazidi kuhesabika kutokana na wimbi la madiwani wa chama hicho kutimkia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Chadema ilifanikiwa kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi kupokonya halmashauri hiyo iliyokuwa ikiongozwa na CCM kwa miaka yote.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, Chadema ilifanikiwa kutwaa halmashauri hiyo na nyingine nchini kupitia nguvu aliyokuwa nayo aliyekuwa mgombea wake urais, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ambaye pia alikiwezesha chama hicho kuongeza idadi ya viti vya ubunge na kupata kura nyingi za urais.

“Hakuna anayeweza kuipuuza nguvu ya Lowassa katika uchaguzi ule na namna alivyokisaidia chama chake kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema mmoja wa wachambuzi hao aliyejitambulisha kwa jina la Jackson Mtindi.

Wakati Chadema mjini Iringa ikiingia katika Uchaguzi wa 2015 ilikuwa na mbunge na diwani mmoja waliochaguliwa katika uchaguzi wa 2010, ilifanikiwa kuzoa viti 14 vya udiwani huku CCM ikiambulia viti vinne tu katika uchaguzi huo wa 2015.

Hata hivyo katika kipindi cha kati ya Oktoba mwaka jana na Januari mwaka huu, Chadema imekwishapoteza madiwani watano wa kuchaguliwa na wawili wa viti maalumu, huku kukiwepo na taarifa zisizo rasmi kwamba wengine wako mbioni kuachana na chama hicho kwa kile wanachodai kushindwa kuvumilia ubabe wa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa.

Kutimka kwa madiwani hao watano, Baraka Kimata wa kata ya Kitwiru, Edger Mgimwa kata ya Kihesa, Joseph Lyata wa kata ya Kwakilosa, Tendesy Sanga wa kata ya Ruaha na Anjelusi Mbogo wa kata ya Mwangata wanaipa CCM nafasi ya kuwa na madiwani wa kuchaguliwa sawa na Chadema, endapo chama hicho kitaendelea kususia chaguzi zote ndogo kama ilivyotangazwa na mwenyekiti wake Freeman Mbowe.

Wakati CCM ikisubiri kuitishwa kwa uchaguzi mdogo katika kata ya Ruaha, Kwakilosa na Mwangata, tayari chama hicho kimekwishainyakua kata ya Kitwiru kupitia uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba mwaka jana na kimepata ushindi usio na jasho kwa mgombea wake July Sawani kupita bila kupingwa baada ya vyama vingine kususia uchaguzi wake mdogo uliokuwa ufanyike Januari 13, mwaka huu.

“Kinachomlinda Mstahiki Meya kwasasa ni madiwani wa viti maalumu ambao Chadema wanao watano na CCM wanaye mmoja. Kwahiyo kama madiwani wengine wanne wa kuchaguliwa wataondoka katika chama hicho, hakuna shaka siku za meya zitakuwa zimefika ukingoni,” alisema mchambuzi mwingine, John Kikoti.

Akizungumzia sakata la madiwani wa chama chake kutimkia CCM, mwenyekiti wa madiwani wa Chadema wa mkoa wa Iringa, Frank Nyalusi alisema; “Hii ni mbinu mpya katika siasa, CCM wanalamba dume, sisi tunalia. Muda wa kuendelea kulia ni lazima uishe kama tunataka kuinusuru hali hiyo.”

Nyalusi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Manispaa ya Iringa anayesubiri hatma yake baada ya kusimamishwa kwa tuhuma za kutaka kukisaliti chama hicho alisema Chadema inatakiwa kubuni mbinu mpya za kuendesha siasa, vinginevyo wananchi wanaweza kukata tamaa.

“Na ni muhimu tukaweka mkakati wa kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi vinginevyo ni bora tuende likizo,” alisema huku akisisitiza kwamba hafikirii wala hashawishiki kujitoa katika chama hicho pamoja na kwamba wenzake wanazidi kufanya hivyo.

“Nitaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Chadema, nimetoka mbali na chama hiki. Sina na wala siioni sababu ya kujitoa na kukimbilia chama kingine,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment