Friday, 26 January 2018

RC MASENZA AMPIGIA MAGOTI FEISAL ASAS

MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amempigia magoti Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Ilambilole, Iringa Vijijini, Bwana Feisal Asas akimuomba asaidie kunyanyua kuta za ama jengo la utawala au mabweni ya shule hiyo.

Kutokana na ukosefu wa majengo hayo, walimu na wanafunzi wa bweni wamelazimika kutumia baadhi ya madarasa ya shule hiyo kwa shughuli za utawala na kama hosteli.

Wakati walimu 26 wanatumia moja ya madarasa ya shule hiyo kwa kazi zao za ualimu, taarifa iliyotolewa na Mkuu wa shule hiyo, Alda Myenzi inaonesha wanafunzi 92 kati ya wanafunzi 392 wa shule hiyo, wakiwemo wasichana 61 na wavulana 31 wanalala madarasani kwasababu ya ukosefu wa mabweni.

Masenza alisema katika moja ya maagizo yake kwa viongozi wa serikali za vijiji vya mkoa huo, aliagiza kila kijiji kiwe na akiba ya tofali 40,000 kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa miradi ya haraka.

Kata ya Kising’a ina vijiji vya Matembo, Kinywang’anga, Igingilanyi ambavyo kwa pamoja vinatarajia kuchangia zaidi ya tofali 120,000 kwa ajili ya ujenzi huo.

Masenza aliahidi kuchangia Sh Milioni moja kwa ajili ya kusimamisha kuta za moja ya majengo hayo huku akipeleka ombi kwa mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo ili naye aweze kusaidia kunyanyua kuta za jengo lingine.

Aliagiza misingi ya majengo hayo iwe imekwishajengwa itakapofika Februari 20, mwaka huu.

Katika ziara yake ya kutembelea shule hiyo, Masenza aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela na baadhi ya viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Iringa wakiwemo waratibu wa Mfuko wa TASAF unaosaidia kaya masikini.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment