Thursday, 25 January 2018

RC MASENZA AKERWA WANAFUNZI ILAMBILOLE SEKONDARI KULALA MADARASANI
MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza ameuagiza uongozi wa kata ya Kising’a wilayani Iringa kuanza mara moja ujenzi wa mabweni katika shule ya sekondari Ilambilole hatua itakayowanusuru  wanafunzi wa shule hiyo wanaolala madarasani.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa shule hiyo, Alda Myenzi inaonesha wanafunzi 92 kati ya wanafunzi 392 wa shule hiyo, wakiwemo wasichana 61 na wavulana 31 wanalala madarasani kutokana na ukosefu wa mabweni katika shule hiyo.

Masenza ametaka ujenzi wa bweni la wavulana na wasichana katika shule hiyo uende sambamba na ujenzi wa jengo la utawala litakalotumiwa na walimu 26 wa shule hiyo ambao pia wanatumia madarsa kufanya kazi zao.

 “Nachotaka kuona ikifika Februari 20 nikute misingi ya majengo yote mawili imejengwa na tofali za vijiji vyote vitatu ziwe hapa kwa ajili ya kunyanyua kuta za majengo hayo. Ole wako nije nikute kazi hiyo haijafanyika, patachimbika na hatutakaa tuelewane,” alisema juzi baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya shule hiyo.

Masenza aliyeahidi kuchangia Sh Milioni moja kwa ajili ya kusimamisha moja kati ya majengo hayo alisema moja ya maagizo aliyowahi kuyatoa kwa serikali za vijiji mkoani Iringa ni kuwa na akiba ya tofali 40,000 kila kimoja kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya ujenzi inayohitaji kufanywa kwa haraka


Pamoja na kuahidi kiasi hicho cha fedha Masenza alisema atamuomba Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, Feisal Abri naye achangie fedha zitakazowezesha kusimamisha jengo moja kati ya majengo hayo huku akimuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Iringa kujiandaa kuyaezeka majengo hayo pindi ujenzi wake utakapokamilika.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment