Tuesday, 30 January 2018

RAILA ODINGA AJIAPISHA KUWA RAIS WA WANANCHI


Kiongozi wa muungano wa upinzani wa Nasa Raila Odinga amejiapisha kuwa ‘Rais wa Watu’ mbele ya maelfu ya wafuasi wake kwenye viwanja vya Uhuru Park miezi mitatu baada ya uchaguzi mkuu anaodai alishinda.

Hata hivyo, wakuu wa muungano huo; mgombea mwenza Kalonzo Musyoka, na vinara Musalia Mudavadi na Moses Wetangula hawakuwepo.

Odinga aliwaambia wafuasi wake kwamba Musyoka ambaye ni wa chama cha Wiper ataapishwa baadaye.

“Mimi Raila Amolo Odinga, kwa kutambua wito mkubwa wa watu natwaa ofisi ya Rais wa Watu wa Jamhuri ya Kenya,” alisema katika kiapo chake chini ya usimamizi wa Mbunge wa Ruaraka Tom J Kajwang.

Baada ya kiapo hicho Odinga alitoa hotuba fupi akisema leo ilikuwa siku ya kihistoria kwa Kenya.

Baada ya kutamka maneno hayo maelfu ya wafuasi wake waliokuwa wamejaa kupita kiasi kwenye viwanja hivyo walilipuka kwa shangwe.

"Tumetimiza ahadi yetu kwa Wakenya,” alisema Odinga kabla ya kuondoka haraka na kuwaacha wananchi wakitoka pia uwanjani hapo.Reactions:

0 comments:

Post a Comment