Monday, 22 January 2018

MUFINDI YAANZA KUJENGA VIWANDA VIPYA, YAZINDUA MKAKATI WAKE WA VIWANDA

MKUU wa wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William amezindua mkakati wa uanzishwaji viwanda vipya katika wilaya hiyo juzi huku kukiwa na viwanda vipya vitano ambavyo ujenzi wake umefikia hatua mbalimbali.

Alivitaja viwanda hivyo kuwa ni pamoja na Bavana Hard Wood Product Plantation kitakachokuwa kikizalisha bidhaa mbalimbali za mbao na ART International Company kinachojishughulisha na uvunaji wa utomvu wa miti kwa ajili ya kutengeneza gundi.

Vingine ni Mkonge Tea Block Farm, kampuni ya wakulima wadogo wa Chai wa kijiji cha Mkonge inayotaka kuingia ubia na kampuni ya CHAI LEO ya Kenya na kujenga kiwanda cha kuchakata chai katika eneo la Chibang’a.

Alivitaja vingine kuwa ni Long Run International cha kutengeneza Playwood ambacho ujenzi wake upo katika hatua ya ufungaji wa mashine na WDF Renewable Resource kitakachoanza hivi karibuni kutengeneza mkaa kwa kutumia vumbi la mbao.

William alisema viwanda hivyo vinajengwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango kazi wa ujenzi wa viwanda vipya 100 mkoani Iringa ifikapo Desemba 2018.

“Sisi tumeanza na ni imani yetu wawekezaji wengine wengi watajitokeza kuwekeza wilayani kwetu hasa kwa kuzingatia uwingi wa rasilimali zilizopo,” alisema.

Wakati viwanda hivyo vipya vikiwa katika hatua za mwisho kuanza uzalishaji, William alisema wilaya yake ina viwanda vingine 84 ambavyo kati yake 14 ni vikubwa, 27 vya kati, na 43 vidogo.

Alisema viwanda hivyo kwa ujumla wake vimetoa ajira 7,323 ambazo kati yake 4,672 ni za kudumu na 2,651 ni za muda.

Akizungumzia maeneo yanayofaa kwa uwekezaji wa viwanda, William alisema yanapatikana katika kata za Isalavanu, Kinyanambo, Rungemba, Changarawe, Bumilayinga, Luhunga, Nyololo, Igowole, Mninga, Ifwagi, Sadani na Malangali.


Alizitaja kazi zilizopangwa kufanywa kati ya Desemba 2017 na kuendelea kuwa ni pamoja na kuainisha, kutembelea na kutenga maeneo ya uwekezaji, kupima maeneo hayo,kufanya vikao na wadau, kuhamasisha uzalishaji wa malighafi za kulisha viwanda na kutangaza fursa zilizopo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment